Main Title

source : Parstoday
Jumapili

20 Novemba 2022

19:58:27
1324952

Amnesty International yaikosoa Marekani kwa kumpa kinga muuaji Bin Salman

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeukosoa utawala wa Rais wa Marekani, Joe Biden, baada ya Ikulu ya White House kutangaza kwamba mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman "ana kinga" inayozuia kushtakiwa katika kesi zinazohusiana na mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.

Shirika hilo pia limeikosoa Riyadh kwa kumteua Bin Salman kuwa waziri mkuu kwa amri ya kifalme, jambo ambalo limezua wasiwasi miongoni mwa wanaharakati wa kutetea haki za binadamu kwamba suala hilo litamlinda mwana mfalme huyo na kumpa kinga ya kusimamishwa kizimbani kutokana ya kesi zote zilizowasiliishwa katika mahakama za nje, ikiwa ni pamoja na kesi iliyowasilishwa na mchumba wa Jamal Khashoggi, Hatice Cengiz, nchini Marekani.

Katibu Mkuu wa Amnesty International, Agnès Callamard amesema katika taarifa yake kwamba: "Serikali ya Marekani inapaswa kuona aibu, na huu ni usaliti wa kuchukiza."

Callamard ameongeza kwamba: "Kwanza, rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alipuuza ushahidi unaomhusisha Bin Salman na mauaji ya Jamal Khashoggi, na kisha Biden ametupilia mbali ahadi yake ya kumfuatilia mwanamfalme huyo." Amesema yote haya yanaashiria "makubaliano ya kutiliwa shaka ambayo yalihitimishwa baina ya pande mbili."

Callamard amesema kuwa hatua hii ya Marekani ya kumpa kinga ya kufikishwa mahakamani Muhammad bin Salman kutokana na mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi ina maana kwamba serikali ya Washington "inatuma ujumbe mbaya kwamba wale walio mamlakani wako juu ya sheria na wanaweza kuhepa kuadhibiwa."

Itakumbukwa kuwa, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imempa kinga Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ili asishtakiwe kwa mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi habari na mkosaji mkuu wa utawala wa Aal Saud. Bin Salman amepewa kinga hiyo licha ya ahadi ya awali ya Rais Joe Biden ya kumwajibisha mtawala huyo wa Saudia kwa jinai hiyo ya kinyama.

Aliyekuwa mchumba wa Jamal Khashoggi, Hatice Cengiz alikuwa amefungua kesi kuhusu mauaji hayo ya kutisha ya Khashoggi katika mahakama ya wilaya huko Washington DC.

Khashoggi aliyekuwa raia wa Marekani na mwandishi habari katika gazeti la Washington Post aliteswa, kuuawa na kisha kukatwa vipande vipande kwa amri ya Muhammad bin Salman. Jamal Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Istanbul, Uturuki. Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) awali lilithibitisha kwamba mtawala huyo wa Saudia ndiye aliyeamuru mauaji hayo.

342/