Main Title

source : Parstoday
Jumapili

20 Novemba 2022

19:59:11
1324953

Kuongezeka maradufu watu wanaokatwa vichwa nchini Saudi Arabia

Serikali ya Saudia inatumia vibaya kimya cha madola makubwa na jamii ya kimataifa, kuzidisha kukata vichwa watu kwa visingizio tofauti kiasi kwamba, idadi ya watu waliotekelezewa adhabu ya kifo na ukoo wa Aal Saud mwaka huu, tayari hivi sasa ni maradufu ya waliokatwa vichwa mwaka jana nchini humo.

Baada ya kukatwa vichwa watu wengine wawili, idadi ya watu waliotekelezewa adhabu ya kifo nchini Saudia tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022 hadi hivi sasa imefikia 138 wakati ambapo mwaka jana idadi hiyo ilikuwa ni watu 69. Tunapolinganisha mwaka huu wa 2022 na mwaka 2020, tutaona kuwa idadi ya watu waliokatwa vichwa nchini Saudia imeongezeka mara tano mwaka huu. Mwaka 2020 watu waliotekelezewa adhabu ya kifo walikuwa 27 kutokana na janga la UVIKO-19 yaani corona.

Ukoo wa Aal Saud unatoa visingizio mbalimbali vya hukumu zake za kifo nchini humo. Baadhi ya hukumu hizo zinatolewa kwa madai ya uhalifu kama wa magendo ya madawa ya kulevya. Kifo ndiyo adhabu wanayopewa wanaofanya magendo ya mihadarati nchini Saudia. Juzi Ijumaa, watu wawili walitekelezewa adhabu ya kifo kwa madai ya magendo ya madawa ya kulevya. Wiki iliyopita pia, watu wengine wawili walikatwa vichwa kwa madai hayo hayo. Kati ya watu hao wanne, ni mmoja tu ndiye aliyekuwa raia wa Saudi Arabia, wengine wote watatu walikuwa raia wa kigeni.

Sababu kuu ya hukumu za kifo nchini Saudia ni masuala ya kisiasa. Idadi ya hukumu hizo imeongezeka sana tangu mfalme Salman na mwanawe bin Salman walipohodhi lijamu ya uongozi huko Saudi Arabia. Adil al Said, naibu wa mkuu wa shirika la Ulaya-Saudia la haki za binadamu, alisema mwezi Aprili mwaka huu kwamba, tangu mwezi Januari 2015 hadi hivi sasa, Salman na mwanawe Mohammed wameshaua maelfu ya watu na hii ni katika hali ambayo, hakuna yeyote kati ya watu hao aliyefanyiwa uadilifu wakati wa kuhukumiwa. Makumi ya wahanga hao walisema mahakamani kwamba walilazimishwa kukiri makosa chini ya mateso makali na ya kinyama.

Mauaji yanayofanywa na serikali ya Saudia ni mengi sana kiasi kwamba, mwezi Machi mwaka huu wa 2022, watu 81 waliuliwa kwa umati siku moja kwa tuhuma za ugaidi huko Saudi Arabia.

Wakati huo viongozi wa Saudia walidai kuwa, watu hao 81 waliouliwa kwa mkupuo siku moja nchini humo, walihusika na vitendo vya ugaidi. Madai hayo yalitolewa katika hali ambayo, ukoo wa Aal Saud hadi sasa umeshindwa kutoa ushahidi madhubuti wa kuhusika watu hao na magenge ya kigaidi.

Ikumbukwe kuwa, ukoo wa Aal Saud unamuhesabu mtu na kundi lolote linalowapinga, kuwa ni kundi la kigaidi. Moja ya makundi yaliyotangazwa kuwa ni ya kigaidi huko Saudi Arabia ni lile la Ikhwanul Muslimin. Ni kwa sababu hiyo pia ndio maana serikali ya Saudia inayahesabu makundi yanayotoka mashariki mwa nchi hiyo ambayo wakazi wake wengi ni Waislamu wa Kishia, kuwa ni ya kigaidi. Wanachama wengi wa makundi hayo wanahukumiwa kifo mara kwa mara nchini humo kwa kulalamikia tu utendaji mbovu wa serikali.

Kwa upande wake, tovuti ya habari ya Harakati ya Ukombozi na Mabadiliko ya Saudi Arabia imefichua kuwa, idadi ya raia wa Saudia waliotekelezewa adhabu ya kifo kutoka mkoa wa Qatif wa mashariki mwa nchi hiyo tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022 hadi hivi sasa imefikia watu 43 huku baadhi yao wakiwa ni Watoto wadogo. Ukoo wa Aal Saud unadai kuwa watu hao wamekatwa vichwa kwa kushirikiana na makundi ya kigaidi, kufanya fujo na kupatikana na silaya ya RPG kwa lengo la kuhatarisha usalama wa nchi.

Kwa kuzingatia yote hayo zikiwemo tuhuma walizopachikwa watu hao za kushirikiana na makundi ya kigaidi, tunaweza kusema kwa kujiamini kwamba, sehemu kubwa ya adhabu hizo za kifo zimetolewa kwa sababu za kisiasa tu huko Saudia. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba madola ya Magharibi na jamii ya kimataifa hasa Umoja wa Mataifa, wote wamekaa kimya kabisa mbele ya jinai hizo.