Main Title

source : Parstoday
Jumapili

20 Novemba 2022

20:00:21
1324955

Kashfa ya uchaguzi Bahrain na uungaji mkono wa London kwa utawala wa Al Khalifa

Watafiti, wanaharakati wapigania mageuzi wa Bahrain na wanaharakati wa jumuiya za kiraia huko London wamefichua kashfa ya uchaguzi wa hivi karibuni huko Bahrain na kutaka kukomeshwa vigezo vya kindumakuwili vya serikali ya Uingereza kuhusu demokrasia na haki za binadamu.

Bi Josie Thum, mtafiti wa ngazi ya juu katika Taasisi ya Haki za Binadamu na Demokrasia huko Bahrain ameeleza kuwa kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa kwa anwani ya "Mchakato Bandia wa Kisiasa", uchaguzi wa hivi karibuni nchini Bahrain ulikuwa wa kimaonyesho kikamilifu katika mtazamo wa kisheria na kisiasa. Ameongeza kuwa, kuna ulazima kufanyika mazungumzo na serikali ya Uingereza na tawala nyingine zinazouhami utawala wa Bahrain ili kuzidisha mashinikizo ya kimataifa kwa utawala huo. 

Duru ya pili ya uchaguzi wa kimaonyesho ilifanyika jana huko Bahrain. Wakati huo huo uchaguzi wa Bunge wa nchi hiyo ulifanyika tarehe 12 mwezi huu, hata hivyo hatima ya karibu viti 35 vya uwakilishi bungeni ilisogezwa katika duru hiyo ya pili ya uchaguzi. 

Bi Rabab Khaddaj, mtafiti wa Taasisi ya Bahrain ya Haki za Binadamu na Demokrasia (Bahrain Insitute for Rights and Democracy) yenye makazi yake huko London amesema: Utawala wa Bahrain umefanya kila uwezalo kudhihirisha ushiriki wa wananchi katika chaguzi za hivi karibuni kwa kubuni takwimu za uongo.  

Ameongeza kuwa, katika hali ambayo nchi za Magharibi, zikiwemo za Marekani na Uingereza, zinaendelea kuuunga mkono utawala kandamizi wa Bahrain; utawala wa Al Khalifa ulizuia kushiriki wanaharakati wa kisiasa na kubana watu na makundi yanayowaunga mkono wanaharakati hao kushiriki katika chaguzi hizo.   

Bi Rabab Khaddaj amesema, utawala wa Bahrain umewapa uraia wa nchi hiyo raia kutoka nchi kama Pakistan na India ili kushiriki katika uchaguzi na kuupigia kura utawala ulioko mamlakani. Mwanaharakati wa kisiasa wa Bahrain ambaye amenyang'anywa uraia wake kwa amri ya utawala wa Al Khalifa amesema kuwa, hivi sasa kuna karibu wafungwa 1,400 wa kisiasa katika jela za Bahrain.

342/