Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

21 Novemba 2022

19:10:43
1325180

Kashfa mpya ya haki binadamu ya serikali ya Marekani

Wizara ya Mahakama ya Marekani imetoa hukumu ya kuishauri serikali ya nchi hiyo kumtoa kwenye hatia Mohamed bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia katika jinai ya mauaji ya kikatili ya Jamal Khashoggi, mwandishi Msaudia aliyekuwa anaukosoa utawala wa nchi hiyo. Khashoggi aliuliwa kinyama kwa kukatwa vipande vipande na maajenti wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki.

Hukumu hiyo ya mahakama ya Marekani imetolewa katika hali ambayo bado kesi iliyofunguliwa na mchumba wa Khashoggi, Bi Hatice Cengiz na Taasisi ya Demokrasia ya Ulimwengu wa Kiarabu dhidi ya mrithi wa ufalme wa Saudia na wenzake, bado iko kwenye mahakama ya shirikisho huko Washington.

Usiku wa kuamkia Ijumaa ya arehe 17 Novemba, 2022, jaji wa mahakama hiyo ya Marekani aliipa muda maalumu serikali ya Joe Biden wa kutoa mtazamo wake kuhusu ombi la wakili wa Bin Salman la kutaka mteja wake huyo atolewe hatiani kutokana na cheo chake kipya. Serikali ya Marekani ingeliweza kukaa kimya tu na isiseme chochote kuhusu suala hilo, lakini haikufanya hivyo.

Vyombo vya habari vya Marekani vimedai kuwa, ingawa ombi hilo halikuwa kitu cha lazima, lakini hatimaye uamuzi wa kutolewa hatiani bin Salman umechukuliwa na jaji, huku serikali ya Biden nayo ikiafiki uamuzi huo.

Licha ya ushahidi mwingi kuonesha kuhusika moja kwa moja Bin Salman katika mauaji ya Jamal Khashoggi, lakini serikali ya Marekani imemtoa hatiani

 

Akionesha hisia zake kuhusu uamuzi huo wa Marekani, Bi Hatice Cengiz, mchumba wa Jamal Khashoggi aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: “Leo Jamal ameuawa tena. Tulidhani kwamba huko Marekani kuna nuru japo ndogo ya kutekelezwa uadilifu, lakini kwa mara nyingine fedha zimedhibiti kila kitu. Hii ndiyo dunia ambayo Jamal na mimi tulikuwa hatuijui…!”

Mwezi Oktoba 2018, mwandishi wa habari Jamal Khashoggi ambaye alikuwa akikosoa utawala wa hivi sasa wa mfalme Salman na mwanawe Bin Salman, aliuawa kinyama ndani ya ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki. Aliuliwa na timu ya mauaji ya Saudi Arabia kwa amri ya moja kwa moja ya Mohamed bin Salman na baadaye mwili wake ulikatwa vipande vipande na hadi hivi sasa vipande vya nyama za mwili wake havijulikani vilipelekwa wapi. Lakini ni kawaida ya Marekani kutochukua hatua yoyote inayopingana na matakwa ya mrithi wa ufalme wa Saudia tangu wakati wa Donald Trump mpaka wakati huu wa urais wa Joe Biden ambao hatimaye umetangaza kuwa Bin Salman hana hatia.

Mwezi uliopita, mfalme Salman wa Saudi Arabia alimteua mwanawe Mohammed bin Salman kuwa mkuu wa Baraza la Mawaziri. Mawakili wa Bin Salman wamedai kuwa, cheo kipya cha mteja wao huo yaani kuwa kwake mkuu wa Baraza la Mawaziri la Saudia, kunampa kinga ya kutofuatiliwa katika mauaji ya Jamal Khashoggi. 

Lakini dunia haijasahau ahadi alizotoa Joe Biden wakati wa kampeni za uchaguzi wa kugombania urais wa Marekani. Aliahidi kuangalia upya uhusiano wa Marekani na utawala wa kiimla wa Saudia iwapo angeliingia madarakani, ili kuandaa mazingira ya kulindwa haki za binadamu. Lakini manufaa ya muda mrefu ya jeopolitiki ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi yameifanya Washington ibadilishe misimamo yake pole pole kuhusu Saudi Arabia.

Baada ya Joe Biden kuingia madarakani mwezi Januari 2021 na viongozi wa Washington kuchukua baadhi ya misimamo iliyoonekana kuwa ni dhidi ya utawala wa ukoo wa Aal Saud, ilitarajiwa kuwa, kutashuhudiwa mabadiliko ya kimsingi katika uhusiano wa Washington na Riyadh. Lakini ahadi zote hizo zilikuwa ni za kudanganya watu tu. Marekani inaihesabu Saudia kuwa ni muitifaki wake mkuu katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Asia Magharibi, hivyo hakuna kiongozi yeyote anayeweza kubadilisha siasa hizo kuu za Washington kuhusu Saudia.

Kwa kweli utendaji wa serikali ya Joe Biden katika suala la haki za binadamu umeonesha wazi kuwa, baadhi ya wakati Marekani inajifanya kuiwekea mashinikizo Saudia. Lakini wakati wowote inapofanya hivyo huwa si kwa sababu Washington ni mkweli katika madai yake, bali ni kwa ajili ya kulikamua zaidi tu gombe la kukamuliwa maziwa kama alivyozoea kuiita hivyo Saudia, Donald Trump, rais wa zamani wa Marekani.

Uhakika daima utabakia kuwa ni ule ule kwamba, Washington haishughulishwi na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa kidikteta wa Saudi Arabia, bali inachojali Marekani ni maslahi yake binafsi tu ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi pamoja na kuulinda utawala pandikizi wa Kizayuni katika eneo hili.

342/