Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

21 Novemba 2022

19:13:27
1325184

Sisitizo la kuchunguzwa jinai za jeshi la Marekani nchini Afghanistan

Sambamba na kuanza uchunguzi kuhusiana na jinai za kivita nchini Afghanistan unaofanywa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetoa wito wa kuchunguzwa mashambulio ya mauaji ya jeshi la Marekani nchini Afghanistan.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, Human Rights Watch imetangaza kuwa, katika miaka 20 ya uwepo wa vikosi vya kigeni nchini Afghanistan, taasisi hiyo ina ushahidi na nyaraka zinazothibitisha kwamba, majeshi ya Marekani yakitegemea ripoti za uongo na kutoa hukumu kabla ya kufahamu ukweli halisi wa mambo, yameua makumi ya raia wa Afghanistan wasio na hatia yoyote.

Sehemu moja ya ripoti ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch inasema: Katika miaka ya 2018 na 2019 ambapo hujuma na mashambulio ya majeshi ya Marekani nchini Afghanistan yaliongezeka na kuchukua wigo mpana raia wengi wa nchi hiyo waliuawa. Kadhalika imekuja katika ripoti hiyo kwamba, kuna ulazima wa kutolewa nyaraka zote zinazoonesha kutekelezwa mashambulio ya usiku nchini Afghanistan hususan katika mashambulio ambayo Shirika la Kijajusi la Marekani (CIA) lilihusika moja kwa moja.

Sisitizo la asasi hiyo ya haki za binadamu la ulazima wa kufuatiliwa na kuchunguzwa jinai za jeshi la Marekani nchini Afghanistan limetolewa sambamba na kuanza uchunguzi kuhusu jinai za kivita za wanajeshi wa nchi hiyo huko Afghanistan unafanywa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). Bila shaka hatua hii ni katika matakwa ya jamii ya kimataifa ya kushughulikiwa faili hili.

Marekani na Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) katika kipindi cha miaka 20 cha kuikalia kwa mabavu Afghanistan walitenda jinai mbalimbali za kivita ambapo matakwa ya wananchi wa nchi hiyo na vilevile fikra za waliowengi ulimwenguni ni kushtakiwa na kupandishwa kizimbani wale wote waliohusika na jinai hii. Licha ya kuweko mashinikizo na vitisho vya Marekani dhidi ya maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuhusiana na kufuatiliwa jinai za jeshi la nchi hiyo huko Afghanistan, lakini kidhahiri inaonekana kuwa, asasi hiyo ya kimataifa imeazimia kutekeleza majukumu yake ipasavyo na ndio maana imeanzisha uchunguzi wa jinai hizo.

Katiika hali ambayo, miito ya kila upande ya kushtakiwa wanajeshi wa Marekani kutokana na kutenda jinai za kivita nchini Afghanistan imeongezeka na kuchukua wigo mpana, wiki iliyopita Kanali ya Televisheni ya BBC ilitangaza katika ripoti yake mpya kwamba, watoto 64 wa Kiafghani wameuawa katika opresheni za kiijeshi za Uingereza katika kipindi cha vita nchini Afghanistan ambapo serikali ya London imekiri na kukubali rasmi matukio 16 tu kati ya hayo. Taasisi moja ya misaada na hisani ya Uingereza imetangaza kuwa, idadi ya raia waliouawa na jeshi la Uingereza nchini Afghanistan ni zaidi ya kile ambacho kimetangazwa hadi sasa. Kwa mujibu wa asasi hiyo ya masuala ya kheri ni kuwa, kuna uwezekano takwimu za watoto waliouawa katika vita nchini Afghanistan ikafikia 135.

Licha ya kuwa wazi kabisa jinai za kivita za wanajeshi wa Marekani na wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) nchini Afghanistan, kukiri viongozi wao na nyaraka zilizofichuliwa na vyombo vya habari vya Magharibi, lakini ikulu ya Marekani White House imekataa katataa kubeba dhima ya hilo na kulipa fidia za jinai hizo kwa familia wahanga wa vita nchini Afghanistan. 

Patrcia Gossman, Mkurugenzi wa Human Rights Watch Kanda ya Asia na mtaalamu wa haki za binadamu nchini Afghanistan anasema:

Marekani na Uingereza wamekwepa mambo mengi kuhusiana na uchunguzi wa kina kuhusu matukio yaliyotokea wakati wa vita nchiini Afghanistan, na hii ina maana kwamba, madola ya Magharibi hayako tayari kutoa majibu ya vitendo vyao kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu na mauaji ya raia hususan wanawake na watoto wadogo nchini Afghanistan.

Shambulio la anga la Marekani dhidi ya hospitali ya Madaktari Wasio na Mipaka katika mji wa Kandahar mwaka 2015 lililosababisha makumi ya watu kuuawa na kujeruhiwa ni moja ya matukio yaliyoko katika faili la Marekani la jinai za kivita nchini Afghanistan ambalo lilifuatiliwa na Bi Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtakaa Mkuu wa zamani wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Kuteswa wafungwa katika magereza ya siri na mashuhuri nchini Afghanistan kama gereza la Begram ni hatua nyingine za kijinai zilizofanywa na wanajeshi wa Marekani ambazo daima zimekuwa zikikosolewa na kulalamikkiwa na asasi za haki za binadamu nchini Afghanistan na katika uga wa kimataifa.

342/