Main Title

source : Parstoday
Jumatano

23 Novemba 2022

17:01:48
1325671

Upotoshaji wa Rais wa Ufaransa kuhusu ukoloni barani Afrika

Katika hali ambayo jinai za Ufaransa katika mataifa mbalimbali barani Afrika zinaendelea kushuhudiwa; Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametahadharisha kuhusiana na satwa na upenyaji wa madola makubwa ya dunia barani Afrika.

Macron ambaye nchi yake ni mtuhumiwa nambari moja wa jinai barani Afrika hasa katika kipindi cha ukoloni ameyatuhumu madola ya kigeni ikiwemo Russia kwamba, inataka kujitanua katika bara hilo. Macron anatoa matamshi hayo katika hali ambayo, kumbukumbu za historia za mataifa mbalimbali katu haziwezi kusahau mauaji ya kutisha na jinai za Wafaransa barani Afrika.

Kinyume na jinsi viongozi wa ikulu ya Elysee wanavyotaka kuonyesha kuwa na sura ya kutoa misaada ya kibinadamu, lakini historia katu haiwezi kusahau mauaji ya kimbari ya Wafaransa dhidi ya wananchi wa Algeria. Jinai hiyo ilikuwa kubwa kiasi kwamba, hivi karibuni Rais Abdelmadjid Tebboune wa Aligeria alitangaza kuwa, mkoloni Mfaransa aliua nusu ya Waalgeria katika jinai zake wakati wa ukoloni, jinai ambayo katu haiwezi kusahauliwa kwa sababu tu ya kupita zama. Muaji ya kimbari ya Rwanda na mauaji ya watu laki nne wa Bamileke nchini Cameroon ni jinai nyingine ambazo licha ya Ufaransa kukana kwamba, haikuhusika, lakini nyaraka kihistoria hazidanganyi.

Kupora madini na utajiri wa mataifa mbalimbali ya Kiafrika, kuwatumikisha Waafrika katika kazi za sulubu na uingiliaji wa kisiasa ni jinai nyingine za Wafaransa katika bara la Afrika.

Katika miongo ya hivi karibuni daima Ufaransa imekuwa na uwepo katika mataifa mbalimbali ya Kiafrika ikitumia visingizio mbalimbali.  Kimsingi ni kuwa, bara la Afrika lina umuhimu maalumu kwa Ufaransa katika nyuga mbalimbali za kiuchumi na kijeshi. Kwa mfano katika uga wa kiuchumi kabla ya mwaka 2020 mashirika ya Kifaransa takribani yalikuwa yakihodhi uzalishaji unaotokana na vyanzo vya madini katika makoloni yake ya zamani kama Niger na Mali.

Katika uga wa kijeshi pia, Ufaransa ina wanajeshi katika nchi mbalimbali za Kiafrika. Si hayo tu bali Ufaransa hata ina kambi na vituo vya kijeshi katika baadhi ya nchi za Kiafrika kama Mali, Niger, Ivory Coast na Chad na kisingizio chake kikubwa cha kuweko katika nchi hizo ni kusaidia juhudi za kurejesha amani na usalama sambamba na kuendesha vita dhidi ya ugaidi.

Hivi sasa pia Ufaransa ina uwepo amilifu katika nchi kadhaa za Kiafarika ikiwa ni katika kalibu ya ukoloni mpya. Kwa muktadha huo, Ufaransa imeendelea kuweko Afrika ikitumia visingizio mbalimbali kama kutoa misaada ya kifedha, mipango ya kiuchumi, biashara, kutoa mikopo, kujenga viwanda na kujenga vituo vya kijeshi.  Katika uwanja huo, viongozi wa Ufaransa nao daima wamekuwa wakifanya safari mara kwa mara barani Afrika ikiwa ni katika juhudi za kuimarisha nafasi na uwepo wa majeshi ya nchi hiyo katika bara hilo na hivyo kutumia fursa hiyo kutekeleza siasa zao kupitia mikataba ya kiuchumi, kijeshi na kisiasa barani humo. Hatua hizo zimekabiliwa na upinzani mkali katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kujitokeza mwamko baina ya wananchi wa mataifa ya Kiafarika. Upinzani huo umekuwa mkubwa kiasi kwamba, katika majuma ya hivi karibuni wananchi wa Burkina Faso walimiminika katika barabara na mitaa mbalimbali ya miji ya nchi hiyo na kuandamana wakilalamikia uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa katika nchi yao. 

Wataalamu wa matukio ya Afrika wanaamini kuwa, madola ya Magharibi yamekuwa yakifuatilia maslahi yao yale yale katika uhusiano wao na nchi za Afrika kama vile kuimarisha zaidi uwepo wao barani humo, kupora mali na utajiri wa madini wa mataifa hayo, kutwisha mipango yao ya kifedha yenye malengo maalumu na kuzusha migogoro ya kijeshi kwa lengo la kuziuzia silaha pande zote zinazozozana.

Licha ya kuwa hii leo kutokana na kuongezeka mwamko wa mataifa harakati ya ukoloni haifuatilii suala la kuanzisha vita na uporaji mali wa moja kwa moja, lakini inafanya njama kupitia mbinu mbalimbali kama misaada kwa mirengo ya upinzani, kuimarisha vyombo vya habari kwa ajili ya propaganda, kueneza uchumi wenye misingi ya matumizi na kubadilisha mtindo wa maisha wa mataifa hayo ya Kiafrika.

Kwa kuzingatia anga na mazingira haya, viongozi wa mataifa ya kikoloni ya Ulaya wakiwa na lengo la kupotosha mambo na kuwafanya walimwengu wasahau machungu na masaibu yaliyosababishwa na ukoloni dhidi ya mataifa ya Kiafrika wamekuwa wakiwatuhumu washindani wao kama Russia na China kwa tuhuma mbalimbali.

342/