Main Title

source : Parstoday
Jumatano

23 Novemba 2022

17:02:51
1325672

Umoja wa Mataifa waendeleza juhudi za kurefusha usimamishaji vita Yemen

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen amesema kuwa umoja huo unaendelea na jitihada zake za kuhakikisha usimamishaji vita unaendelezwa nchini humo.

Makubaliano ya kusimamisha vita ambayo muda wote yalikuwa yanavunjwa na muungano vamizi wa Saudia na Imarati, yalifikiwa kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa na yaliongezewa muda mara mbili na muda wake ulimalizika tarehe pili Oktoba.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Hans Grundberg akisema hayo katika kikao maalumu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, juhudi za Umoja wa Mataifa za kuridhisha pande hasimu zinaendelea. Ujumbe wa umoja huo umetumwa San'a na Riyadh kufuatilia suala la kurefushwa usimamishaji vita huko Yemen.

Saudia na kundi lake vamizi wamefanya ukatili mkubwa nchini Yemen

 

Aidha amesisitiza kuwa, sambamba na mabadliko ya kijeshi na kiuchumi, kuna udharura kwa mazungumzo ya hivi sasa kufikia natija ya haraka sana. Hali iliyopo hivi sasa ni tete na kuna wajibu wa kurefushwaa haraka makubaliano ya kusimamisha vita. Matatizo ya kiuchumi na kibinadamu hayawezi kutatuliwa bila ya kupatiwa ufumbuzi kwanza masuala ya kiusalama na kukomeshwa mapigano.

Mwezi Machi 2015, Saudia kwa kushirikiana na baadhi ya madola ya Kiarabu hasa Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati), ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya nchi maskini ya Yemen kwa msaada na baraka kamili za madola ya Magharibi kama Marekani, Uingereza na Ufaransa. 

Muungano huo vamizi ulikuwa na ndoto ya kumaliza vita vya Yemen katika kipindi kifupi tu, lakini muqawama wa wananchi wa Yemen umewakwamisha kwenye kinamasi kizito na licha ya kupita miaka saba ya mashambulizi ya pande zote na vikwazo vya kila upande, lakini wananchi wa Yemen wamesimama kidete na kufelisha ndoto za wavamizi hao.

342/