Main Title

source : Parstoday
Jumatano

23 Novemba 2022

17:05:48
1325675

Raia wa Ghana waliofutwa kazi na Twitter wadai haki za sheria ya kazi

Wafanyakazi wa Twitter waliofutwa kazi nchini Ghana wameripotiwa kuajiri wakili na kutuma barua kwa kampuni hiyo ya Marekani kuitaka ifuate sheria za kazi za ndani ya Ghana.

Miongoni mwa madai ya kundi hilo ni kupata mshahara kamili wa miezi mitatu baada ya mkataba wa kazi kufutwa na malipo mengine yanayolingana na yale yanayopokewa na wafanyakazi wa Twitter duniani kote.

Kwenye barua hiyo ambayo pia imesambazwa kwenye vyombo vya habari, wafanyakazi hao wamesema: "Ni wazi kwamba Twitter, chini ya mmiliki wake mpya Elon Musk, inakiuka sheria za Ghana kwa makusudi au kwa uzembe, inafanya kazi kwa nia mbaya na kwa njia ambayo inalenga kuwanyamazisha na kuwatisha wafanyikazi wa zamani kukubali masharti yoyote ambayo wanayopewa.”

Wafanyakazi hao pia wameiomba serikali ya Ghana kuilazimisha Twitter "kufuata sheria za nchi hiyo kuhusu kuachisha watu kazi na kufanya mazungumzo ya haki na uadilifu na waliofutwa kazi sambamba na kutoa malipo wanayopata wale wanaoachishwa kazi."

Aidha katika taarifa wamesema: "Wafanyikazi wamefadhaika, wamefedheheshwa na wanatishwa na mabadiliko yaliyojiri. Kuna wafanyakazi wasio raia wa Ghana, baadhi wakiwa na familia changa, ambao walihamia hapa kufanya kazi na sasa wameachwa bila kujali gharama za kuwarejesha nyumbani na hakuna njia ya kuwasiliana na Twitter kwa ajili ya kujadili kesi yao.”

Wiki moja tu baada ya Elon Musk kununua kampuni hiyo, Twitter iliwafuta kazi takriban wafanyakazi wake wote nchini Ghana, na kubakisha mmoja tu. Hata hivyo, wafanyakazi waliofukuzwa hawakupata malipo yoyote ya kuachishwa kazi kwa mujibu wa sheria za kazi za Ghana na mikataba ya ajira ya Twitter. Zaidi ya hayo, wafanyakazi wa Ghana walilalamika kwamba hawakufahamishwa kuhusu kufutwa kazi kwa wakati, tofauti na wafanyakazi nchini Marekani na Ulaya.

Baada ya kuchukua kampuni hiyo Musk alianza kuwafuta kazi wafanyikazi ulimwenguni mnamo Novemba, zaidi ya wiki moja baada ya kuchukua jukumu. Inadokezwa kuwa wafanyakazi 7,500 wamefutwa kazi Twitter na waliobakia sasa ni takribani 2,700 tu.

342/