Main Title

source : Parstoday
Jumatano

23 Novemba 2022

17:10:41
1325684

Boko Haram waua askari 10 wa Chad katika mpaka wa Nigeria

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram wamewaua wanajeshi 10 wa Chad katika eneo la mpakani baina ya nchi hiyo na Nigeria.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Chad imesema kuwa, kundi la Boko Haram limeshambulia kikosi cha jeshi katika eneo la Ziwa Chad karibu na mpaka wa nchi hizo mbili na kuua wanajeshi kumi wa Chad.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kitengo hicho cha jeshi kilikuwa kikijenga kambi ya kijeshi ya Jeshi la Chad katika kisiwa cha Boka Tolorum wakati kiliposhambuliwa na kundi la Boko Haram. 

Katika miaka ya hivi karibuni Nigeria imekumbwa na mashambulizi ya umwagaji damu ya magenge mbalimbali hususan kundi la kigaidi la Boko Haram. Mashambulizi haya kwanza yalianza kaskazini mwa nchi na kisha kuenea katika maeneo mengine ya Nigeria.

Kundi la kigaidi la Boko Haram lilishika silaha mwaka 2009 kwa lengo la kujiimarisha kaskazini mwa Nigeria na baadaye lilipanua mashambulizi yake hadi katika nchi za Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon.

Zaidi ya watu 30,000 wameuawa na karibu wengine milioni tatu wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya kundi hilo.

342/