Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

24 Novemba 2022

18:46:32
1325942

Kuanza urutubishaji wa urani wa asilimia 60 katika kituo cha Fordo; radiamali ya Iran kwa hatua za uhasama za Magharibi

Ikiwa ni katika kujibu azimio la hivi karibuni la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran limetangaza uzalishaji wa urani iliyorutubishwa hadi kiwango cha asilimia 60 katika kituo cha Fordo.

Shirika la Nishati ya Atomiki linataka kutumia kituo hicho katika kuandaa na kuzalisha urani iliyorutubishwa kwa kiwango hicho cha juu. Vyombo vya habari viliripoti Jumatatu kwamba Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran pia limetayarisha na kuingiza gesi katika mitambo mingine miwili ya IR2M na IR4 katika kituo cha Natanz, na hivyo kuimarisha shughuli zake za nyuklia katika kituo hicho, yote hayo yakiwa yanafanyika kwa malengo ya amani.

Hatua madhubuti ya Iran ya kuongeza kiwango cha urutubishaji wa urani hadi asilimia 60 imechukuliwa katika hali ambayo awali Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, alikuwa ametangaza kwamba Tehran ingechukua "hatua kadhaa" kama jibu kwa hatua ya hivi karibuni ya nchi tatu za Ulaya na Marekani ya kupitisha azimio dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya IAEA.

Siku ya Jumanne, Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, alithibitisha kurutubishwa urani kwa asilimia 60 huko Fordo na kusema: "Katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia kupitishwa azimio dhidi ya Iran, ambalo limekabiliwa na radiamali yetu, ambapo katika siku za karibuni uzalishaji wa urani ya Uf-6 iliyorutubishwa hadi asilimia 60 umeanza.

Siku ya Alhamisi, Novemba 17, Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki iliidhinisha azimio lililopendekezwa na Marekani na Troika ya Ulaya, ambapo Iran ilishutumiwa kutotoa ushirikiano wa kutosha kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya nyuklia. Hii ni mara ya pili mwaka huu kwa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kupitishia azimio dhidi ya Iran kuhusu suala hilo hilo. Azimio la kwanza lilipitishwa mwezi Juni 2022. Katika miaka ya karibuni wakala wa IAEA umekuwa ukifuatilia na kukariri baadhi ya madai yanayotolewa na utawala haramu wa Israel kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na kuitaka Tehran ijibu madai hayo yasiyo na msingi.

Hii ni katika hali ambayo mwaka 2015, na ikiwa ni katika fremu ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na vile vile mapatano ya "PMD" ambayo yanazuia utumiwaji wa nishati ya nyuklia katika masuala ya kijeshi, Iran ilitoa majibu ya kutosha na ya kukinaisha kwa wakala huo. Hivi sasa wakala huo umeomba ukaguzi ufanyike katika baadhi ya maeneo na vituo vya nyuklia vya Iran ili kukidhi matakwa ya utawala haramu wa Israel. Kuhusiana na hilo, katika azimio la karibuni Baraza la Magavana limeitaka Tehran ishirikiane na wakala huo kuhusu maeneo yanayotiliwa shaka ya Marivan, Varamin na Torquzabad. Tehran imeyachukulia madai hayo kuwa ya uwongo na kuyapuuzilia mbali.

Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema kwamba Tehran imetoa majibu marefu na ya kina kuhusu maswali yaliyoulizwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, lakini wakala huo unatoa ripoti zake kutokana na taarifa zilizopokelewa kutoka kwa maadui wa Iran.

Mohsen Naziri, Mwakilishi wa Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA amepinga azimio la karibuni la Baraza la Magavana dhidi ya Iran na kusema: Malengo ya kisiasa ya waandaaji wa azimio hilo hayatatimia, na kupitishwa kwake kunaweza kuathiri mchakato wa ushirikiano mzuri uliopo kati ya Iran na Wakala."

Hatua madhubuti za Iran katika kupanua urutubishaji wa asilimia 60, ambalo linachukuliwa kuwa jibu kwa hatua za kiuadui za nchi za Magharibi dhidi ya Tehran, zimekabiliwa na majibu hasi kutoka kwa nchi hizo. Troika ya Ulaya imetoa taarifa ya pamoja ikilaani maendeleo ya nyuklia ya Iran na kusisitiza: "Tutaendelea kushauriana na washirika wetu wa kimataifa kuhusu njia bora ya kukabiliana na uimarishaji wa mpango wa nyuklia wa Iran."

Kwa hakika, kupitishwa kwa azimio jipya lililowasilishwa na Marekani na Troika ya Ulaya katika Baraza la Magavana ni jaribio la nchi za Magharibi la kuongeza mashinikizo dhidi ya Iran zikidhani kwamba kutokana na machafuko ya Iran kwa upande mmoja na mkwamo uliopo sasa katika mazungumzo ya Vienna na sisitizo la Marekani la kutokubali matakwa ya Iran kuondolewa vikwazo, kwa upande wa pili, kunaweza kuilazimisha Tehran kukubali matakwa yao yasiyo ya kimantiki na ya kulazimishwa kupitia mashinikizo ya kisiasa, au Iran kulazimika kufumbia macho haki zake halali na za kisheria.

Hii ni katika hali ambayo hatua ya Iran kuamua kusimama imara na kustawisha shughuli zake za uruni inathibitisha wazi kwamba haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya nchi za Magharibi kwa njia yoyote ile.

342/