Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

25 Novemba 2022

18:05:24
1326149

Onyo kali la Yemen kwa muungano wa Saudia kuhusu kuendelea kuporwa nishati ya nchi hiyo

Huku uporaji wa mafuta ya Yemen ukiwa unaendelea, Abdul Aziz bin Habtour, Waziri Mkuu wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen ametahadharisha kuwa, iwapo uporaji huo utaendelea, Wayemen watalazimika kuzilenga meli za mafuta za muungano wa Saudia.

Vikosi vya jeshi la Yemen siku ya Jumatatu viliilazimisha meli ya mafuta iliyokuwa inapanga kukaribia bandari ya al-Dabbah, iliyoko mashariki mwa mji wa Makla, mji mkuu wa mkoa wa Hadhramaut (mashariki mwa Yemen), kuondoka kwenye bandari hiyo. Bandari hiyo inakaliwa na mamluki wa muungano vamizi wa Saudia na Imarati. Meli hiyo ilikuwa inapanga kupora mapipa milioni mbili ya mafuta ya Yemen.

Yemen ni mojawapo ya nchi maskini zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu. Hali ya umaskini na njaa nchini humo imezidi kuwa mbaya katika kipindi cha miaka 8 iliyopita wakati muungano wa Saudia unaendeleza vita vya kichokozi dhidi ya nchi hiyo. Mbali na  muungano huo kufanya uharibifu mkubwa huko Yemen kutokana na mashambulio yake ya kijeshi ambapo raia wengi wa nchi hiyo wameuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kuishi kama wakimbizi kwenye nchi yao wenyewe, muungano huo ungali unaisababishia nchi hiyo hasara kubwa ya kiuchumi kwa kuyakalia kwa mabavu maeneo ya mashariki na kusini mwa nchi kwa sababu rasilimali za nishati ya Yemen zinapatikana katika maeneo hayo.

Moja ya mikakati ya serikali ya Saudia na Imarati huko Yemen ni kuyakalia kwa mabavu maeneo muhimu ya nchi hiyo na kupora rasilimali zake. Nchi hizo vamizi zimechukua hatua hiyo ili, kwa upande mmoja, ziweze kuwa na ushawishi wa kisiasa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, na kwa upande mwingine, ziweze kupora rasilimali za nishati ya nchi hiyo masikini.

Kwa mujibu wa Abdul Aziz bin Habtour, muungano wa Saudia na Marekani umepora zaidi ya dola bilioni 14 za mapato ya mafuta na gesi ya Yemen na kuziweka kwenye Benki ya Kitaifa ya Saudi Arabia. Muungano wa Saudia unapora mali ya Yemen, yakiwemo mafuta, huku watu wa nchi hiyo wakiwa katika hali mbaya zaidi ya kibinadamu duniani, jambo ambalo maafisa wa Umoja wa Mataifa pia wamekuwa wakiliashiria na kuonya mara kwa mara kuhusu madhara yake.

Suala jingine kuhusu kuporwa rasilimali za nishati za Yemen na muungano wa Saudia ni kwamba makampuni ya Magharibi pia yako katika muungano huo. Kuhusiana na hilo, Ibrahim as-Sarraji, katibu wa habari wa Kamati Kuu ya Kiuchumi ya Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen, aliwaita wawakilishi wa makampuni ya kimataifa na kuwatahadharisha kuhusu jaribio la kusafirisha mafuta kutoka bandari ya al-Dhaba katika mkoa wa Hadhramout. Hii inaonesha kuwa Wamagharibi wanashirikiana moja kwa moja na Saudia na Imarati katika kupora rasilimali za nishati ya Yemen. Katika miezi ya hivi karibuni, ripoti kadhaa zimechapishwa kuhusu kuhamishwa nishati ya Yemen kwenda Ulaya.

Kwa kuzingatia muendelezo wa mchakato huo, Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen imeonya kwamba itachukua hatua za kijeshi dhidi ya meli za mafuta zinazopora mafuta ya nchi hiyo. Abd al-Aziz bin Habtour, Waziri Mkuu wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen, alisema Jumanne, akikusudia shambulio la tahadhari lililofanyika karibuni karibu na meli ya mafuta ya kigeni iliyokuwa ikijaribu kuiba mafuta ya Yemen kwamba: "Wakati ujao, hatutaionya meli yoyote, bali tutailenga moja kwa moja." Bin Habtoor ameongeza kuwa: "Dunia nzima inapaswa kujua kwamba hatutaruhusu watu wetu wafe njaa ilihali muungano wa Saudia na Marekani wanapora utajiri wa Yemen."

Ni wazi kwamba ikiwa muungano wa Saudia hautalichukulia kwa uzito onyo hilo la Waziri Mkuu wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa na kuendelea kupora rasilimali zake za nishati, vita vya Yemen vitaongezeka tena hivi karibuni.

342/