Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

26 Novemba 2022

18:36:03
1326427

"Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulibadilisha mlingano wa nguvu duniani"

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya jana hapa Tehran amesema Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulibadilisha kabisa mlingano wa nguvu kieneo na kimataifa.

Hujjatul Islam Mohammad Javad Haj Ali Akbari alisema hayo jana katika hotuba za Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyoongozwa na Imam Khomeini MA yameweza kuvunja njama zote za maadui dhidi ya Iran katika kipindi cha miongo minne iliyopita sambamba na kuibua mlingano mpya katika eneo la Asia Magharibi na dunia nzima kwa ujumla.

Hujjatul Islam Haj Ali Akbari amesisitiza kuwa, mzozo mkubwa uliopo baina ya Iran na madola ya kibeberu ni ustawi wa Jamhuri ya Kiislamu, kwani maadui hawataki kuliona taifa hili likipiga hatua za maendeleo.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya jana hapa Tehran ameashiria fujo na ghasia za hivi karibuni hapa nchini na kueleza bayana kuwa, miongozo aali ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei imesaidia pakubwa kurejesha amani, usalama na utulivu hapa nchini.

Amesisitiza kuwa, "Kiongozi Muadhamu amesema wazi kuwa, hii leo, ni wajibu wa kila mtu kufanya bidii kwa ajili ya maeneleo ya nchi hii, na kila mwenye ghera na Iran hana budi ila kujipinda kwa ajili ya ustawi wa nchi hii."

Katika sehemu nyingine ya hotuba zake, Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amegusia juu ya kuwadia Wiki ya Basiji na kueleza kuwa, jeshi hilo la kujitolea lililoasisiwa na  Imam Rouhoullah Khomeini MA, limekuwa na mchango chanya na athirifu katika masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiutamaduni hapa nchini.

Amesema jeshi la Basiji lililoundwa siku 22 tu baada ya wananchi wa Iran kudhibiti Pango la Ujasusi la Marekani wakati Mapinduzi ya Kiislamu yalipoingia kwenye makabiliano ya moja kwa moja na Washington, limekuwa mstari wa mbele pia kuidhaminia nchi hii amani na usalama.   

342/