Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

26 Novemba 2022

18:36:31
1326428

IRGC yaongeza wanajeshi katika mpaka wa magharibi wa Iran

Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametangaza habari ya kutumwa wanajeshi zaidi katika mipaka ya magharibi na kaskazini magharibi mwa Iran ili kupiga jeki operesheni za kukabiliana na makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga yaliyoko katika eneo la Kurdistan nchini Iraq.

Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour alisema hayo jana Ijumaa na kusisitiza kuwa, lengo la kutumwa vikosi zaidi katika maeneo hayo ya mpakani ni kuzuia kujipenyeza nchini magaidi kutoka nchi jirani ya Iraq.

Brigedia Jenerali Pakpour ameeleza bayana kuwa,  vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi hii vitaendelea kulilinda taifa hili kutokana na vitisho vya kutoka nje ya mipaka yake.

Kamanda huyo wa kikosi cha nchi kavu cha SEPAH amesisitiza kwamba, jeshi hilo litaendeleza operesheni za nchi kavu dhidi ya makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga yaliyoko katika eneo la Kurdistan nchini Iraq hadi tishio hilo litakapotokomezwa na kupokonywa silaha magaidi hao.

Hivi karibuni, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilianza duru mpya ya mashambulizi dhidi ya makundi ya kigaidi yanayotaka kujitenga baadhi ya maeneo ya Iran yenye makao yake katika eneo la Kurdistan ya Iraq.

Mashambulizi hayo yalifanyika kwa makombora na ndege zisizo na rubani za kamikaze kwenye viunga vya mji wa Kirkuk.  Tehran imetahadharisha katika siku za karibuni kwamba, iwapo serikali ya Baghdad haitochukua hatua dhidi ya makundi hayo, basi Iran haitakuwa na budi ila kuendeleza mashambulizi dhidi ya makundi hayo katika eneo la Kurdistan nchini Iraq.

342/