Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

26 Novemba 2022

18:37:03
1326429

Uungaji mkono wa Marekani kwa makundi yanayotaka kujitenga ya Iran

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imelaani operesheni za kijeshi Iran dhidi ya makundi ya kigaidi ya Wakurdi wanaotaka kujitenga yaliyoko kaskazini mwa Iraq na imeitaka Tehran kusitisha mashambulizi hayo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa taarifa hiyo baada ya Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) kutoa malalamiko yake kuhusiana na operesheni za kijeshi za Iran dhidi ya makundi hayo katika eneo la Kurdistan ya Iraq. Ned Price, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, alidai katika taarifa hiyo kwamba: "Hatua ya Iran ya kuingia kinyume cha sheria ndani ya ardhi ya Iraq inaendelea kupitia mashambulizi mabaya dhidi ya eneo la Kurdistan la Iraq kuanzia tarehe 20 hadi 22 Novemba." Kwa mujibu wa tovuti ya wizara hiyo, Price alidai: "Marekani inalaani vikali ukiukaji huo wa mara kwa mara na usio na huruma wa ardhi ya Iraq na inatoa wito kwa Iran kujiepusha na vitisho na ghasia zaidi." Awali pia, Michael Erik Kurilla, kamanda wa CENTCOM alisema katika taarifa yake kwamba: "Tunalaani mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani ya Iran ya kuvuka mpaka karibu na Erbil nchini Iraq."

Uungaji mkono wa waziwazi wa Marekani kwa makundi ya Wakurdi wanaotaka kujitenga nchini Irani ambayo yameanzisha kambi na vituo vingi vya uendeshaji na mafunzo katika eneo la Kurdistan la Iraq na yanayovuruga usalama katika maeneo ya mpaka na kufanya mashambulizi ya silaha dhidi ya walinzi wa mpaka wa Iran kwa shabaha ya kutimiza malengo ya ubeberu wa kimataifa unaoongozwa na Marekani, unaonyesha sura halisi ya mienendo ya kiuadui na uhasama wa Washington dhidi ya Iran. Maafisa wa serikali ya Marekani wamezungumzia mara kwa mara ulazima wa kuigawa Iran. Lengo lao ni kwamba, kupitia njia ya kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, wataweza kuigawa nchi hii ambayo ina historia ya ustaarabu wa maelfu ya miaka, katika maeneo ya kikabila, ili kwa utaratibu huo Iran ya Kiislamu ambayo ni kizingiti na changamoto kubwa dhidi ya sera za kibeberu na ubabe wa Marekani, iwe imefutwa katika kanda na duniani.

Wamarekani wamekuwa wakifuatilia utekelezaji wa mpango huo kwa muda mrefu. Kwa mara ya kwanza baada ya Vita vya Pili vya Dunia, James Francis Byrnes, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wakati huo alichora ramani na kuigawa Iran katika sehemu 7 kulingana na makabila au kaumu zake. Wakati huo, Byrnes alidhani kuwa Iran sio nchi muhimu katika milinganyo ya siasa za dunia, kwa hivyo aliwasilisha mpango wa kuigawa katika nchi 7 ndogo.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, juhudi za Marekani za kuigawa Iran ziliwekwa tena kwenye ajenda ya nchi hiyo. Mpango wa "Mashariki ya Kati Kubwa" wa Bernard Lewis, profesa mzayuni wa chuo kikuu huko Marekani, pia unasisitiza udharura wa kugawanywa nchi za eneo la Magharibi mwa Asia. Lewis anasema: "Nchi za Kiislamu ni tishio kwa Ulimwengu wa Magharibi na nchi hizi lazima zigawanywe ili nguvu ya Uislamu iangamizwe mara moja na milele, vinginevyo Uislamu utaiangamiza Magharibi." Sehemu muhimu na kuu ya mpango wake ilikuwa kuigawa Iran: "Kulingana na mpango wa Lewis, Iran itagawanywa katika sehemu 6. Kwa hakika, sehemu za Iran zitaungana na nchi jirani, na kaumu za Kibaloch, Kiarabu, Kituruki, na Kikurdi zitajitenga na Iran.

James George Jeters, mmoja wa washauri wa zamani wa Baraza la Seneti la Marekani anasema: "Israel na Saudi Arabia zinataka kuangamiza nguvu ya kikanda ya Iran, na mojawapo ya masuluhisho yao ni kuigawa Iran na kuipasua vipande vipande."

Kwa njia hii, Marekani, ikiwa ni shetani mkubwa na adui mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, daima imekuwa ikifanya mikakati ya kutekeleza mpango wake wa uadui wa kuigawa Iran, na katika suala hili inatoa uungaji mkono wa pande zote kwa makundi ya wanaotaka kujitenga nchini Iran, yakiwemo makundi ya Kikurdi kama vile Komala, PAK na PAJAK.

Hata hivyo, hatua madhubuti za Iran na mashambulizi yake mengi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi na vituo vya makundi hayo huko Kurdistan ya Iraq ni pigo kubwa kwa stratijia ya Marekani na ni hatua madhubuti ya kufifisha mipango ovu ya Washington dhidi ya Iran ya Kiislamu. Marekani ambayo kwa sasa imejikita katika kuzusha machafuko na ghasia nchini Iran, inayaona makundi hayo yanayotaka kujitenga kama kielelezo cha utekelezaji wa sera hiyo ya serikali ya Washington.

342/