Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

26 Novemba 2022

18:40:55
1326432

Sudan Kusini yajitoa kwenye mazungumzo ya amani na makundi ya waasi

Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kujiondoa rasmi kwenye mazungumzo ya amani na makundi ya waasi ikiyatuhumu makundi hayo kwamba, yamekuwa yakipoteza muda huku yakijiandaa kwa vita.

Sudan Kusini imesema hayo katika barua iliyoandikwa hivi karibuni kwa Shirika la Kikatoliki la Mtakatifu Egidio. Waziri anayehusika na masuala ya rais, Barnaba Marial Benjamin ambaye pia ni kiongozi wa ujumbe wa serikali ya Juba katika mazungumzo hayo amesema kuwa, serikali ya Sudan Kusini imesitisha ushiriki wake katika mazungumzo ya amani ya Roma kwa muda usiojulikana.

Mazungumzo kati ya serikali na muungano wa makundi ya waasi ambayo hayakutia saini makubaliano ya amani ya mwaka 2018 yaliyohitimisha vita vya wenyewe kwa wenyewe, yalifanyika mjini Roma Italia kwa kusimamiwa na shirika moja la kikatoliki lililo na mafungamano na Vatican. Mazungumzo yalianza mwaka 2019 ingawa machafuko hayajasita kusini mwa nchi hiyo licha ya kutiwa saini makubaliano ya kusitisha vita Januari 2020. 

Nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ilitumbukia kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu makamu wake wakati huo, Riek Machar kuwa alipanga njama ya kumpindua.

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kwa kupiga kura ya maoni iliyoungwa mkono na asilimia 99 ya raia wake baada ya vita vya miongo kadhaa vya kupigania kujitenga. Inasadikiwa kuwa Sudan Kusini ilichochewa na madola ya kibeberu kujitenga na Sudan.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimeshasababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

342/