Main Title

source : Parstoday
Jumapili

27 Novemba 2022

16:50:01
1326735

Njama na hila za adui wa taifa la Iran za kulazimisha JCPOA 2 na JCPOA 3

Baada ya Iran na nchi zilizounda kundi la 5+1 kufikia mwafaka Julai 2015 juu ya kadhia ya nyuklia ya Iran na kusaini Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, kwa kifupi JCPOA, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, -iwe ni baada ya kuanza kutekelezwa JCPOA mnamo mwaka 2016 au baada ya kujitoa Marekani kwenye makubaliano hayo Mei 2018, na hata katika kipindi cha sasa kufuatia duru kadhaa za mazungumzo ya Vienna ya uondoaji vikwazo vya kidhalimu-

kila mara zimekuwa zikilazimisha masuala mengine yasiyohusiana na JCPOA, hususan ya silaha za makombora ya Iran na sera zake za kikanda, yajadiliwe chini ya anuani ya JCPOA 2 na JCPOA 3.

Muelekeo huu wa Wamagharibi umekuwa kila wakati ukikabiliwa na jibu kali la Iran. Viongozi waandamizi wa Jamhuri ya Kiislamu wamesisitiza mara kadhaa kuwa Iran inapinga kufanya mazungumzo ya aina yoyote kuhusu maudhui zingine ghairi ya nyuklia na hasa kuhusiana na silaha zake za makombora na sera na hatua inazochukua katika kadhia za eneo hili hususan uungaji mkono wake kwa mhimili wa Muqawama na makundi ya Jihadi katika nchi za Lebanon, Yemen, Palestina na Syria. Lakini pamoja na hayo, kila pale Wamagharibi wapatapo fursa na kisingizio, hukitumia kuibua dai lao hilo ambalo si la kisheria na halina uhusiano wowote na JCPOA.

Japokuwa rais Joe Biden wa Marekani alisikika mara kadhaa akitoa ahadi kabla na baada ya uchaguzi wa rais wa Novemba 2020 ya kuirejesha nchi hiyo kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lakini ushahidi uliopo, muelekeo na misimamo iliiyoonyeshwa na Washington hadi sasa inaonyesha kuwa, ukweli hasa ni kwamba Marekani haina nia ya kurudi kwenye makubaliano hayo.

Hata kama kujitoa Washington kwenye JCPOA mnamo mwaka 2018 kulitangazwa na Donald Trump, lakini ukweli unabaki kuwa yeye alifanya hivyo kama mwakilishi wa utawala wa Marekani; na hatua yake hiyo iliakisi takwa la Washington. 

Uhakika wa mambo ni kuwa Wademocrat na Warepublican wana mtazamo mmoja juu ya suala kwamba, mapatano ya 2015 ya JCPOA hayakidhi maslahi ya Marekani. Na ndio maana Washington inahaha kuanzisha JCPOA 2 na JCPOA 3; na mirengo yote miwili ya Wademocrat na Warepublican inataka, mbali na kadhia ya nyuklia, yafanyike mazungumzo na Iran juu ya masuala mengine pia. Bila shaka tafsiri ya mazungumzo iliyomo akilini mwa viongozi wa Marekani si ya majadiliano baina ya pande mbili zenye sauti sawa na kila upande kutoa na kupewa kitu ili ufikiwe mwafaka wa pamoja. Mazungumzo inayokusudia Washington ni yale yatakayoiwezesha kuitwisha Tehran matakwa yake na kutekelezewa kila itakalo bila nayo kutoa chochote kwa Iran. Hakuna shaka yoyote kuwa Iran haiwezi kamwe kukubali mazungumzo ya aina hiyo ya upande mmoja na yasiyo na insafu; na hii ni moja ya sababu za kutofikiwa mwafaka katika mazungumzo ya Vienna ya uondoaji vikwazo. 

Vyama vyote viwili vya Democrats na Republican vina mtazamo mmoja kuhusiana na njama ya kuanzisha JCPOA 2 na 3, isipokuwa zinatafautiana katika mbinu na njia ya kulifikia lengo hilo. Warepublican wanasema, inapasa JCPOA 1, 2 na 3 zipatiwe mwafaka kwa mpigo; yaani Washington ifanye mazungumzo mara moja tu na Iran na kufikia makubaliano juu ya masuala yote. Lakini mtazamo wa Wademocrat ni kwamba, lengo la Washington dhidi ya Iran inapasa lifuatiliwe hatua kwa hatua, lakini mirengo yote miwili inakubaliana kwamba mazungumzo na Iran lazima yavuke mpaka wa kadhia ya nyuklia; na hata katika kadhia hiyo pia Washington isikubali kurejea kwenye JCPOA ya mwaka 2015, bali iuwekee mipaka na masharti mapya mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameashiria katika hotuba na miongozo yake kadhaa kuhusu njama na dhamira ya Marekani na waitifaki wake ya kutaka kuitwisha Iran JCPOA nyingine na akatahadharisha juu ya suala hilo. Katika hotuba yake ya jana Jumamosi Novemba 25 aliyotoa mbele ya hadhara ya wapiganaji wa kujitolea, Basiji, Ayatullah Khamenei alitoa ufafanuzi kuhusu lengo la adui la kutekeleza njama ya JCPOA 2 na 3; ambapo mbali na kutanabahisha kuwa mgogoro wa Iran na Marekani hautatatuka kwa mazungumzo alisema: "baadhi ya wanaojifanya wajuzi wa siasa wanasema, ili fujo zimalizike, inapasa mtatue matatizo yenu na Marekani...suali ni vipi tatizo letu na Marekani litaweza kutatuka? Tatizo litatatuka kwa kufanya mazungumzo na kupewa ahadi?" Ayatullah Khamenei alibainisha kwamba, nia ya adui ilikuwa ni kufikia kwenye JCPOA 2 na 3. JCPOA 2, maana yake ni Iran ijiondoe katika eneo. JCPOA 3, maana yake ni Iran itoe ahadi kwamba haitaunda silaha yoyote muhimu ya kitsratejia. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza kwa kusema: "mazungumzo hayatatua mgogoro wetu na Marekani".

Kwa muktadha huo, na kwa kuzingatia msimamo mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambao imeshazitangazia mara kadhaa pande za Magharibi katika mazungumzo ya Vienna na pia Marekani kupitia mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana, Tehran haitakubali katu kufanya mazungumzo ya aina yoyote ile ya kutekeleza upya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mkabala wa kuondolewa vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa; na wakati huohuo inataka ipewe hakikisho na Washington kwamba haitajitoa tena kwenye makubaliano hayo. Isitoshe, mazungumzo pekee itakayokubali kufanya Iran ni ya JCPOA ya 2015 na haitajadili maudhui yoyote iliyo nje ya mduara huo.../