Main Title

source : Parstoday
Jumapili

27 Novemba 2022

16:52:00
1326737

Kustawisha uhusiano na kutatua hitilafu na majirani; kipaumbele cha sera za nje za serikali mpya ya Iraq

Mohammed Shia al Sudani Waziri Mkuu mpya wa Iraq amefanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi kwa kuzitembelea Jordan na Kuwait.

Waziri Mkuu mpya wa Iraq Jumatatu iliyopita alielekea Jordan akiwa katika ziara yake ya kwanza rasmi nje ya nchi. Shia al Sudani si Waziri Mkuu wa kwanza wa Iraq kuwahi kufanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi huko Jordan. Huko nyuma pia, Noury al Maliki aliitembea Jordan katika duru yake ya awali akiwa Waziri Mkuu wa Iraq.  

Kupakana kijiografia Iraq na Jordan ni miongoni mwa  sababu zilizowapelekea mawaziri wakuu wawili wa Iraq kuichagua Jordan kama sehemu ya ziara zao za kwanza nje ya nchi.  Iraq na Jordan aidha zina mpaka wa pamoja wenye urefu wa kilomita 180. Sababu hii ya kijiografia na pia utambulisho wa pamoja wa Kiarabu baina ya nchi hizo ndizo zilizotoa msukumo kwa nchi mbili hizo kuchukua hatua za kustawisha uhusiano kati yazo. 

Kustawisha uhusiano wa kiuchumi na kufanya mashauriano kuhusu masuala mbalimbali ya kikanda pia ni kati ya malengo ya ziara ya al Sudani huko Jordan. Uhusiano kati ya Jordan na Iraq ulipiga hatua wakati wa utawala wa Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq Mustafa al Kadhemi; na nchi mbili pamoja na Misri ziliitisha vikao vya pande tatu mara kadhaa. Mustafa al Kadhemi Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq na Waziri Mkuu wa Jordan, Bisher Al-Khasawneh mwezi Oktoba uliopita waliweka jiwe la msingi la mradi wa kuunganisha umeme kati ya nchi mbili katika eneo moja karibu na mpaka wa nchi hizo.  

Hii ni katika hali ambayo, Jumatano iliyopita al Sudani pia alifanya safari yake ya pili nje ya nchi akiwa katika wadhifa huo wa Waziri Mkuu wa Iraq kwa kuelekea nchini Kuwait. Kuwait nayo ina mpaka wa pamoja na Iraq wenye urefu wa kilomita 254. Ziara ya Mohammed Shia al Sudani huko Kuwait baada ya ile ya Jordan inaashiria wazi azma ya serikali mpya ya Iraq ya kustawisha uhusiano na nchi jirani. Kuhusiana na hilo, katika safari yake huko Kuwait Shia al Sudani amesema: Iraq inataka kuwa na uhusiano wenye uwiano na majirani zake kwa msingi wa kuheshimiana pande mbili na kulinda mamlaka ya kujitawala ya nchi mbili na kwamba nchi hizo zinafanya juhudi ili kuyapatia ufumbuzi masuala mengi kwa mujibu wa maslahi ya pamoja na kwa lengo la kudumisha amani na uthabiti katika eneo. Al Sudani ameashiria suala la kutatua kadhia mbalimbali katika uhusiano kati ya Iraq na Kuwait kwa kuzingatia hitilafu za jiopolitiki zilizopo kati ya nchi mbili hizo. 

Wakati huo huo vyombo vya habari vya Iraq Alhamisi iliyopita vilitangaza juu ya kukaribia safari ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mohammed Shia al Sudan katika nchi tatu yaani Iran, Uturuki na Saudi Arabia. Safari hizo tarajiwa zinaashiria namna serikali mpya ya Iraq inavyotoa kipaumbele katika sera zake za nje kuhusu suala la kustawisha uhusiano na kutatua hitilafu na majirani zake. Ziara hizo vile vile zinabainisha wazi kwamba, Iraq inataka kuwepo sera zenye uwiano ambapo kwa mujibu wa sera hizo hakutakuwa na mhimili unaopingana na mhimili mwingine. 

Nukta nyingine ni kuwa serikali mpya ya Iraq pia inafanya jitihada za kuendelea kuwa mpatanishi kati ya Iran na Saudi Arabia. Kuhusiana na hilo, Jumatano iliyopita kulitolewa taarifa zikielekeza kuhusu uwezekano wa viongozi wa kisiasa wa Saudia na Iran kufanya mazungumzo huko Baghdad. Ammar al Faiz Mkuu wa Kamati ya Uhusiano wa Nje katika Bunge la Iraq pia amesisitiza katika mazungumzo na gazeti la al Arabi al Jadid kwamba, ujumbe wa upatanishi kati ya Tehran na Riyadh utaendelea kupitia serikali ya al Sudani; kwa sababu uhusiano mzuri kati ya Iran na Saudi Arabia una manufaa kwa Iraq. Kwa msingi huo, Waziri Mkuu mpya  wa Iraq Mohammed Shia al Sudani atakamilisha mradi huo tajwa wa upatanishi kati ya nchi mbili hizo. 


342/