Main Title

source : Parstoday
Jumapili

27 Novemba 2022

16:52:23
1326738

Katibu Mkuu wa UN apongeza mkutano wa Angola kuhusu amani na usalama DRC

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha matokeo ya mkutano wa viongozi kuhusu amani na usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mkutano uliofanyika Luanda Angola tarehe 23 mwezi huu wa Novemba kwa mwaliko wa Rais wa taifa hilo João Lourenço.

Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, amemnukuu Katibu Mkuu akikaribisha pia uamuzi uliotokana na mkutano huo ambao ni kuweko kwa sitisho la mapigano na wakati huo huo waasi wa M23 kuondoka mara moja maeneo ambayo wanashikilia.

Mkutano huo ulioitishwa na Rais Lourenço wa Angola, ulihudhuriwa na Rais Evariste Ndayishimiye, Rais wa Burundi na mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, Rais Felix Tshisekedi, wa DRC, Vincent Biruta, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda akimwakilisha Rais Paul Kagame na Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye ni Msuluhishi aliyeteuliwa na EAC kwenye mchakato wa amani DRC.

Katibu Mkuu ameongeza sauti yake kwa wale waliotia saini taarifa ya pamoja ya mkutano huo na kutoa wito kwa jeshi la DRC na vikundi vya kigeni vilivyojihami kuweka silaha zao chini na kuanza mara moja mchakato wa kusalimisha silaha, kuvunja makundi, kujumuika kwenye jamii na kurejea makwao vile inavyoonekana inafaa.

Kama ilivyoombwa na watiaji saini kwenye taarifa hiyo ya pamoja, Katibu Mkuu amesisitiza uwepo wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO katika kusaidia utekelezaji wa makubaliano hayo kwa mujibu wa mamlaka yake na utayari wa kuratibu na jeshi la kikanda la Jumuiya ya Afrika MAshariki, EAC ili kutoa usaidizi wa haraka wa mfumo wa uthibitishaji utakaondwa kwa mujibu wa Mpango wa Luanda na wakati huo huo kuendelea kusaidia mchakato wa Nairobi kuhusu amani na usalama DRC.

Katibu Mkuu pia amesisitiza uwepo wa Umoja wa Mataifa katika kusaidia kurejea makwao kwa wakimbizi wa ndani kwa uratibu na mamlaka husika chini ya mifumo iliyoko, na sambamba na sheria na kanuni za kibinadamu za kimataifa.

342/