Main Title

source : Parstoday
Jumanne

10 Januari 2023

15:37:40
1337452

Kukamatwa majasusi 13 wa Mossad nchini Iran

Wizara ya Intelijensia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imegundua timu 6 za operesheni za kijasusi za shirika la utawala haramu wa Israel Mossad, na kuwakamata mahasusi 13 wa shirika hilo la kijasusi na kigaidi.

Wizara ya Intelijensia ya Iran imetangaza kuwa mnomo Disemba 22 ilifanikiwa kugundua timu nne za operesheni za shirika la kijasusi na kigaidi la Mossad, na kwamba sasa timu hizo zimeongezeka na kufikia 6.

Tangazo hilo limeongeza kuwa katika mtandao huo wa kigaidi, kulikuwa na majasusi 23 waliokuwa wakiendesha operesheni na kulisaidia shirika la Mossad katika mikoa ya Tehran, Isfahan, Yazd, Azarbaijan Magharibi na Golestan nchini Iran, na kwamba hadi sasa watu 13 waliokuwepo ndani ya nchi wamekamatwa na vifaa vyao mbalimbali vya ugaidi vimegunduliwa na kunaswa.

Taarifa ya Wizara ya Intelijensia ya Iran inasema kuwa, mkuu wa mtandao huo kwa jina bandia la Sirus, amekuwa akiishi katika moja ya nchi za Ulaya ambako amekuwa akifanya mawasiliano ya awali na wahusika wa operesheni za kigaidi ndani ya Iran kupitia mitandao ya kijamii ya Instagram na WhatsApp.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shirika la kijasusi na kigaidi la Mossad, lilikuwa limepanga kutumia vibaya fursa ya machafuko ya hivi karibuni katika baadhi ya maeneo ya Iran, kumuua afisa mmoja wa kijeshi na kutekeleza operesheni kadhaa za hujuma na uharibifu katika miji mikubwa ya Iran, pamoja na kutuma kiwango kikubwa cha vilipuzi na mabomu katika mipaka ya bahari ya kusini mwa nchi ambapo magaidi wote waliohusika katika operesheni hizo walitambuliwa na kukamatwa kabla ya kutekeleza operesheni hizo.

Wizara ya Intelijensia ya Iran imebainisha katika taarifa hiyo kwamba, hilo ni tukio la pili kubwa la kushindwa kiujasusi na kioperesheni utawala bandia na haramu wa Israel katika kipindi cha chini ya miezi 6, ambapo kama kawaida, umekabiliwa na jibu kali na madhubuti la taifa shujaa, jasiri, kenye mwamko na la kujitolea la Jamhuri ya Kislamu ya Iran.

Kuibuliwa machafuko ya hivi karibuni katika baadhi ya miji ya Iran kwa kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini kwa mara nyingine tena kumewatia tamaa maadui wa kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuwafanya wayatumie kama fursa ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran na kuchochea ghasia zaidi.

342/