Main Title

source : Parstoday
Jumatano

11 Januari 2023

16:58:06
1337780

Iran yamuita balozi wa Iraq kulalamikia utumiaji wa neno bandia la Ghuba ya Uajemi

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuita balozi wa Iraq mjini Tehran, kulalamikia kitendo cha mamlaka za Baghdad kutumia neno bandia la 'Ghuba ya Kiarabu' badala ya 'Ghuba ya Uajemi' katika mashindano ya kandanda ya nchi za Kiarabu, yanayoendelea katika mji bandari wa Basra, kusini mwa Iraq.

Hayo yamesemwa leo Jumatano katika taarifa na Hossein Amir- Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye amefafanua kuwa, Nasir Abdul Mohsen Abdullah, balozi wa Iraq mjini Tehran ameitwa katika wizara hiyo kubainishiwa malalamiko rasmi ya Iran, baada ya mamlaka za Iraq kutumia neno bandia kuashiria Ghuba ya Uajemi.

Abdollahian amesema kuwa, Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia Al-Sudani hivi karibuni alitumia neno hilo bandia la Ghuba ya Kiarabu katika ujumbe alioutuma katika mitandao ya kijamii, lakini baadaye akalazimika kusahihisha ujumbe huo na kutumia neno halisi na sahihi la Ghuba ya Uajemi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, licha ya taifa hili kuwa na uhusiano mzuri, wa kina na wa kistratajia na Iraq, lakini limelazimika kubainisha wazi malalamiko yake kwa kupindishwa neno hilo.

Ghuba ya Uajemi

Wakati huohuo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Tehran imewasilisha rasmi malalamiko yake kwa Iraq hasa ikizingatiwa kuwa, Ghuba ya Uajemi siku zote itasalia kuwa Ghuba ya Uajemi; na matamshi yanayotolewa na maafisa wa serikali za nchi ajinabi au kuendesha mashindano ya michezo kivyovyote vile haviwezi kubadilisha uhakika huu wa kihistoria.

Umoja wa Mataifa umetoa taarifa kadhaa na kubainisha kuwa, taasisi za nyaraka na ramani za kijiografia zimetaja bahari iliyo kusini mwa Iran kuwa ni Ghuba ya Uajemi.

Viongozi wa Iran wamesisitiza mara chungu nzima kuwa, hata kama eneo hilo litapachikwa majina mengine bandia mara nyingi, lakini Ghuba ya Uajemi daima itabakia kuwa ni ya Uajemi.   

342/