Main Title

source : Parstoday
Jumatano

11 Januari 2023

16:58:59
1337782

Kan'ani: Mashinikizo ya juu zaidi ya Marekani dhidi ya Iran yamefeli

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema uadui wa Marekani kwa Jamhuri ya Kiislamu si jambo geni, na kwamba tawala zote za Marekani zimekuwa zikifuata sera ya "mashinikizo ya juu" dhidi ya Iran.

Katika msururu wa ujumbe wa Twitter jana Jumanne, Nasser Kan’ani amesema kampeni ya "mashinikizo ya hali ya juu kabisa" ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa katika ajenda ya marais wote wa Marekani kwa kisingizio cha uongo cha kutetea haki za binadamu na demokrasia. Ameongeza kuwa, "lakini hawajafanikiwa chochote zaidi ya kushindwa kabisa."

Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Iran ameendelea kwa kujohji hivi,  "Kwa nini Wamarekani hawajifunzi kutokana na kashfa zote zinazosababishwa na imani yao kwa washauri wa Israel ambao ni wasaliti na wanafiki?" Aidha amesema leo Iran imeendelea kubakia kuwa nchi huru na yenye kujitegemea ambayo ina uwezo mkubwa.

Matamshi hayo ya Kana’ani yamekuja siku moja baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei kusema kwamba amepokea hati mpya iliyofichuliwa inayoonyesha kuwa kuwa rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter aliiamuru CIA mwezi Disemba 1979 kuipindua Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Ujumbe katika akaunti ya Twitter ya Kiongozi Muadhamu amesema kuwa: "Hii ina maana wamekuwa na nia hii tangu kuanzishwa kwa Mapinduz ya Kiislamu. Hati hiyo inataja propaganda kama njia ya kuyapindua Mapinduzi.”

Amri hiyo ya utendaji ilitolewa kwa mara ya kwanza na Jimmy Carter mnamo Novemba 4, 1979, miezi kadhaa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyouangusha utawala kibaraka wa kifalme wa Pahlavi uliokuwa ukiungwa mkono na Marekani nchini Iran. Amri hiyo imekuwa ikitekelezwa kwa miaka 42 na marais waliofuata wa vyama vya Republican na Democratic. Marekani na Jamhuri ya Kiislamu hazikuwa na uhusiano wa kidiplomasia tangu 1980. Marekani pia imeiwekea Iran vikwazo vya kibiashara tangu mwaka 1995.

342/