Main Title

source : Parstoday
Jumatano

11 Januari 2023

17:00:47
1337786

Ujumbe wa ngazi za juu wa Oman wawasili Sana'a, Yemen

Duru za habari za Sana'a mji mkuu wa Yemen zimeripoti kuwa ujumbe wa ngazi ya juu wa Oman umewasili mjini humo kufuatilia suala la kurefushwa usitishaji vita nchini Yemen.

Duru hizo za habari zimesema, ujumbe huo wa ngazi ya juu wa Oman uliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a, mji mkuu wa Yemen jana kwa lengo la kukamilisha mazungumzo kuhusu matukio ya hivi karibuni ya nchini Yemen ikiwa ni sehemu ya jitihada za kurefusha muda wa usitishaji vita na kuleta amani.

Kabla ya hapo pia yaani tarehe 21 Disemba 2022, ujumbe wa Oman ulielekea pia Yemen ili kuwasilisha mapendekezo mapya ya kuongeza muda wa usitishaji mapigano na kuleta amani. Mohammad Abdus Salam, mmoja wa viongozi wa harakati ya Ansarullah na mkuu wa timu ya mazungumzo ya serikali ya Sana'a amesema kuwa, lengo la safari ya ujumbe wa Oman huko Yemen ni kuwasilisha fikra na mapendekezo yaliyowasilishwa katika mazungumzo yao kwa Saudia na mataifa mengine. 

Amesema: Muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia na Marekani haukuheshimu ahadi zake. Wanatoa kauli tupu kuhusu malipo ya mishahara, kuacha kuizingira Yemen na kuondolewa wanajeshi vamizi nchini humo.

Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya Yemen tarehe 26 Machi 2015 ikishirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu hasa Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kwa baraka kamili za Marekani na uungaji mkono wa pande zote utawala wa Kizayuni wa Israel. Mashambulio hayo ya kivamizi  yamesababisha zaidi ya watu 47,000 kuuawa na kujeruhiwa. 

Usitishaji vita nchini Yemen ulifikiwa mwezi Aprili mwaka jana 2022 kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa na umeongezewa muda mara mbili. Makubaliano hayo yalitarajiwa kuongezewa muda tena mwezi Oktoba 2022 lakini upuuzaji wa muungano vamizi na kutoheshimu kwake makubaliano hayo kumekwamisha kuongezewa muda hadi hivi sasa.

342/