Main Title

source : Parstoday
Jumanne

31 Januari 2023

15:52:59
1342715

Russia yalaani shambulio lililofeli la droni dhidi ya kituo cha kijeshi cha Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amelaani shambulio la ndege zisizo na rubani (droni) dhidi ya kituo cha kijeshi cha Iran katika mji wa Isfahan, katikati ya Iran.

Maria Zakharova amesema shambulio hilo lililogonga mwamba la hivi karibuni dhidi ya kambi ya Wizara ya Ulinzi ya Iran yumkini likachochea taharuki isiyoweza kudhibitika katika eneo la Asia Magharibi.

Amesema vitendo vya aina hiyo vinaweza kuibua matokeo mabaya kwa usalama na uthabiti wa eneo hili. Zakharova ametoa onyo kali kwa wahusika wa njama hizo na washirika wao, akisisitiza kuwa, mashambulio kama hayo yenye lengo la kuidhoofisha Iran hayatazaa matunda. 

Wizara ya Ulinzi ya Iran ilitangaza usiku wa kuamkia Jumapili kuwa, jengo moja la karakana za Wizara ya Ulinzi mjini Esfahan lililengwa na shambulio lililofeli la ndege tatu ndogo zisizo na rubani aina ya Micro Air Vehicle (MAV), ambapo moja ya droni hizo ilitunguliwa, nyingine ilinaswa kwenye mtego wa mitambo ya ulinzi wa anga na droni tatu iliangukia kwenye paa la karakana hiyo na kuripuka.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Intelijensia wa Iran, Esmail Khatib amesema hatua zinazochukuliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hili na nchi jirani zinaashiria namna utawala huo ulivyoishiwa na kukata tamaa.

Amesema utawala wa Kizayuni licha ya propapaganda nyingi, lakini unadidimia na kusambaratika ndani kwa ndani, na mfano wa wazi wa migogoro ya kisiasa ndani ya utawala huo, na wimbi la vipigo kutoka kwa makundi ya muqawama wa Palestina.


342/