Main Title

source : Parstoday
Jumatano

1 Februari 2023

18:45:41
1342983

Maandamano ya 'watu milioni moja' Ufaransa kupinga mpango wa pensheni wa Macron

Ufaransa ilikabiliwa na matatizo makubwa ya usafiri siku ya Jumanne huku maandamano ya nchi nzima yakifanyika kwa mara ya pili nchini kote katika muda wa chini ya mwezi mmoja kwa lengo la kulazimisha serikali kuachilia mbali mpango tata wa pensheni.

Takriban wafanyikazi milioni moja wameshiriki katika duru ya pili ya mgomo wa kitaifa dhidi ya mpango wa Rais Emmanuel Macron wa kuongeza umri wa chini wa kustaafu kutoka miaka 62 hadi 64 kama sehemu ya mpango wa mageuzi.

Umri wa kisheria wa kustaafu nchini Ufaransa kwa sasa ni 62 - chini kuliko ilivyo katika nchi nyingi zilizoendelea, ikiwa ni pamoja na sehemu kubwa ya Ulaya na Marekani.

Zaidi ya watu milioni mbili waliandamana katika miji ya Ufaransa mnamo Januari 19 kulalamikia mpango huo wa serikali. Mgomo huo ulisimamisha treni, mbali na kufungwa mitambo ya kusafisha petroli na kuzuia uzalishaji wa umeme katika nchi hiyo ya Ulaya.

Polisi wa Ufaransa walitumia gesi ya kutoa machozi na virungu kutawanya maandamano hayo, ikiwa ni pamoja na katika mji mkuu, Paris.

Vyama vikuu vya wafanyakazi nchini humo viliitisha mgomo wa siku ya pili Januari 31 katika jaribio la kumshinikiza Macron na serikali yake kubatilisha mipango hiyo.

Mgomo wa wafanyakazi katika sekta tofauti mnamo Jumanne ilisimamisha treni na metro au treni ya chini ya ardhi na pia kupunguza uzalishaji wa umeme. Kulingana na chama kikuu cha walimu, karibu nusu ya walimu wote wa chekechea na shule za msingi pia waligoma.

Kampuni ya Reli ya Kitaifa ya Ufaransa (SNCF) ilitangaza kuwa usafiri wa kati ya miji ulitatizwa pakubwa kwani ni treni moja tu kati ya treni tatu za mwendo kasi ilikuwa kazini.

Vyama vya wafanyakazi vikiongoziwa na chama kikuu cha wafanyakazi, CGT,  vinatumai ushiriki wa waandamanaji zaidi ya milioni moja katika miji zaidi ya 200 kote Ufaransa utaishinikiza zaidi serikali isikileze matakwa yao.

Ongezeko la umri wa chini wa kustaafu hadi 64 kutoka miaka 62 ya sasa ni sehemu kuu ya mpango wa mageuzi uliosukumwa na Macron ili kuhakikisha ufadhili wa siku zijazo wa mfumo wa pensheni wa nchi.

Wakati vyama vya wafanyakazi vimekaribisha utayarifu wa serikali kwa mazungumzo kuhusu sehemu za mpango huo, vinasema sheria iliyopendekezwa ya miaka 64 lazima ifutwe.