Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

3 Februari 2023

12:41:07
1343304

OIC yaitisha kikao kulaani kuchomwa moto Qur'ani Tukufu

Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeitisha imelaani jinai iliyofanywa na baadhi ya watu wenye misimamo mikali barani Ulaya ya kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu. hatua hiyo imechukuliwa katika kikao cha OIC ambacho kimejadili hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya watenda jinai hao.

Hivi karibuni kumeshuhudiwa vitendo vya kukivunjia heshima kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani, huko Uholanzi, Sweden na Denmark; jinai ambayo imewakasirisha sana Waislamu duniani kote.   

Katika kikao hicho kilichofanyika Jeddah nchini Saudi Arabia, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya OIC Hussein Ibrahim Taha amelaani kitendo hicho cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu kilichofanywa na baadhi ya watu wenye misimamo ya kuchupa mipaka na kukitaja kuwa cha kichochezi.  

Ibrahim Taha ameeleza kuwa, jinai hiyo dhidi ya Waislamu ilikusudiwa kwa lengo la kuidhalilisha dini Tukufu ya Uislamu na kuyavunjia heshima matukufu na thamani za Waislamu. 

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) pia amezitolea wito serikali za nchi husika kuwachukulia hatua kali wale wote waliotenda jinai hiyo.

Ibrahim Taha ameongeza kuwa, kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu ni kuwavunjia heshima na kuwadhalilisha moja kwa moja Waislamu bilioni moja na milioni 600 kote duniani.   

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki, Misri, Kuwait, Imarati, Al Azhar ya Misri, Jumuiya ya Kimataifa ya Maulamaa wa Kiislamu, Qatar, Saudi Arabia, Indonesia, Jordan, Morocco, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, harakati ya Ansarullah ya Yemen, Harakati ya Hizbullah ya Lebenon, Hamas, na Jihad al Islami za Palestina ni kati ya nchi na taasisi zilizolaani waziwazi kitendo hicho cha kukera na kutaka kuzuia kukaririwa hujuma hiyo na kuadhibiwa wahusika. 

Nchi na taasisi hizo pia zimetahadharisha kuhusu kuongezeka kwa vitendo vinavyopelekea kuvunjiwa heshima dini nyinginezo na kushadidisha machafuko. 

342/