Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

3 Februari 2023

12:41:47
1343305

Radiamali ya Iran kwa vitendo vya uhasama vya utawala wa Kizayuni na msimamo wa kichochezi wa Ukraine

Amir Saeed Irwani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, siku ya Jumatano, akizungumzia shambulio la kigaidi kwenye kiwanda cha Wizara ya Ulinzi huko Isfahan, amesema katika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na pia kwa mwenyekiti wa kiduru wa Baraza la Usalama kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa utawala wa Kizayuni umehusika na tukio hilo la kigaidi.

Amesema hatua hiyo ni ugaidi ambao unakiuka wazi sheria za Kimataifa na kuulaani vikali. Barua ya mwakilishi huyo wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, inafafanua wazi msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mzozo unaoendelea huko Ukraine na kusisitiza kuhusu hatua ya serikali ya Tehran ya kutoegemea upande wowote katika mgogoro huo na kutaka kuheshimiwa kujitawala, uhuru na umoja wa ardhi ya nchi hiyo. Wakati huo huo imeeleza malalamiko na kusikitishwa Iran na kauli ya kichochezi na isiyo na msingi iliyotolewa na afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Ukraine kuhusu shambulio la kigaidi lililofanyika karibuni kwenye kiwanda cha Wizara ya Ulinzi ya Iran ambapo alikaribisha matumizi ya nguvu dhidi ya miundombinu muhimu ya Iran. Balozi Irwani amesema matamshi ya afisa huyo ni ishara ya kutowajibika kwake na ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na misingi inayofuatwa katika Umoja wa Mataifa na kulitaka Baraza la Usalama la umoja huo lililaani matamshi hayo.

Msimamo thabiti wa Iran dhidi ya hatua za kiuadui za utawala wa Kizayuni na uchochezi wa Ukraine, ambao umebainishwa kwa njia ya barua rasmi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa unaonyesha kuwa, Tehran inatambua kikamilifu vitendo vya maadui na waitifaki wao na inafuatilia kikamilifu mienendo yao na kuchukua hatua za lazima kwa wakati unaofaa. Hii si mara ya kwanza kwa Tel Aviv kuchukua hatua za uharibifu na za kichokozi dhidi ya Iran. Utawala wa Kizayuni ukiwa adui mkubwa wa kieneo wa Iran, mbali na kujaribu kuanzisha muungano wa kieneo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, umejaribu kutekeleza vitendo vya mapinduzi na uharibifu ndani ya Iran kupitia vibaraka wake.

Ingawa mauaji ya wasomi na wanasayansi, milipuko katika viwanda na vitendo vingine vya ugaidi ni miongoni mwa mbinu ambazo zimetumiwa na majasusi wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni (Mossad) dhidi ya Iran katika miaka ya hivi karibuni, lakini mara nyingi mipango hiyo ya ujasusi na ugaidi imegonga mwamba baada ya kugunduliwa mapema na hatimaye kuvunjwa na wataalamu shupavu wa masuala ya usalama wa Iran. Kwa mfano mwaka uliopita, utawala huo ulijaribu kushambulia kituo kimoja huko Isfahan kwa ushirikiano wa vibaraka wake wa kundi linalotaka kujitenga la Komoleh lakini wakagunduliwa mapema na kukamatwa pamoja na vifaa vyao vya ujasusi na silaha. Wakati huo huo Iran imetoa ushahidi wa wazi kuhusu kuhusika utawala wa Kizayuni katika shambulizi la hivi karibuni katika kiwanda cha Wizara ya Ulinzi huko Isfahan.

Katika barua yake, balozi wa Iran ameashiria matamshi ya rais wa utawala wa Kizayuni katika makao makuu ya NATO Januari 27 na mkuu wa majeshi ya utawala huo Januari 16 kuhusu tishio la kutumia nguvu dhidi ya miundombinu nyeti ya Iran, ikiwemo ya matumizi ya amani ya nyuklia, na kulalamikia vikali ukiukahi huo wa sheria za kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa. Balozi Irwani amenukuu matamshi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni, katika mahojiano ya hivi karibuni na CNN mnamo Januari 31, ambapo alikiri kuhusika utawala huo katika vitendo vya ugaidi dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa utawala huo unapaswa kuwajibishwa kutokana na jinai na vitendo vyote vya ugaidi ulivyotenda dhidi ya Iran na kukubali matokeo yake bila kufanyiwa upendeleo wowote.

Suala jingine ni msimamo wa uchochezi wa Ukraine katika kuunga mkono shambulio lililofanyika katika kituo cha Wizara ya Ulinzi huko Isfahan. Mykhailo Podolyak, mshauri wa rais wa Ukraine, aliandika ujumbe kwenye ukurasa wake binafsi kwenye Twitter kwa maneno ya chuki, akitangaza kushiriki Kyiv katika shambilio hilo la kigaidi katika kiwanda cha Wizara ya Ulinzi huko Isfahan. Jumapili, Januari 29, alitaja tukio hilo lililotekelezwa Jumapili asubuhi kuwa ni "Usiku wa milipuko nchini Iran" na kuwaambia viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran: "Ukraine imewaonya. "Kama maneneo hayo ya mshauri wa rais wa Ukraine, ambayo yalionyesha kushiriki Kyiv moja kwa moja katika shambulio hilo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hayangekanushwa rasmi na serikali ya Ukraine, ni wazi kuwa serikali hiyo ingebebeshwa lawama na matokeo ya matamshi hayo yasiyokuwa ya uwajibikaji.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema mara kwa mara kwamba ina haki ya kimsingi, kwa mujibu wa sheria za kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa, kutetea usalama wake wa kitaifa na kutoa jibu kali na madhubuti kwa tishio lolote, mahala popote na wakati wowote inaoona kuwa unafaa. Wakati huo huo, Tehran inasisitiza kuwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia hati ya umoja huo na kulaani matamshi ya kivita yanayotolewa mara kwa mara na watawala wa Kizayuni na kuutaka utawala huo ufuate sheria za kimataifa na kusimamisha harakati zake hatari na haribifu katika eneo.


342/