Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

3 Februari 2023

12:43:19
1343308

Iran yakosoa ripoti 'isiyo sahihi' ya IAEA kuhusu kituo cha Fordow

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amelalamikia ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu shughuli za nyuklia za kituo cha nyuklia cha Fordow nchini Iran na kusema tafsiri ya mkaguzi wa IAEA aliyetembelea kituo hicho cha nyuklia haikuwa sahihi.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya nyuklia siku ya Jumatano liliishutumu Iran kwa kufanya mabadiliko ambayo hayajatangazwa kwenye muunganisho kati ya makundi mawili ya mashine za hali ya juu zinazorutubisha madini ya uranium hadi kufikia kiwango cha asilimia 60 katika kituo chake cha Fordow.

Mohammad Eslami, mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) alisema jana Alhamisi kuwa, "Msimamo wa IAEA ni wa kusikitisha."

Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa maonyesho ya mafanikio ya hivi karibuni ya nchi katika uwanja wa tasnia ya nyuklia, Eslami ameeleza kuwa tafsiri ya mkaguzi wa IAEA ya ukaguzi wa Fordow haikuwa sahihi, lakini waliripoti mara moja kwa wakala.

Aidha ameongeza kuwa, Iran ilitoa maelezo mara moja kwa IAEA na mkaguzi wa wakala aligundua kuwa walifanya makosa.

Mnamo Novemba, Iran ilituma barua kwa IAEA kuifahamisha juu ya uamuzi wa kuanza kurutubisha urani hadi kiwango cha usafi cha asilimia 60 katika kituo chake cha nyuklia cha Fordow.

Eslami amesema maonyesho hayo yanalenga kuthibitisha kwamba asili ya mafanikio ya nyuklia ya nchi hii ni tofauti kabisa na yale ambayo nchi za Magharibi zinadai kuhusu malengo yasiyo ya amani ya kazi ya nyuklia.

Ameongeza kuwa Iran inakusudia kuzalisha asilimia 20 ya umeme wake kupitia nishati ya nyuklia.

Mkuu wa nyuklia wa Iran pia amesema kuwa matumizi ya nishati ya nyuklia katika nyanja za matibabu, mazingira, afya na usalama wa chakula yako kwenye ajenda ya shirika hilo.

342/