Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

4 Februari 2023

11:34:28
1343514

Mpakistan Majid Khan aachiwa huru na Marekani baada ya mateso na kusota gerezani Guantanamo kwa miaka 20

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imetangaza kuwa Majid Khan, mfungwa Mpakistani ambaye alifichua jinsi alivyoteswa na shirika la ujasusi la Marekani CIA baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, amehamishwa kutoka gereza la Guantanamo Bay nchini Cuba na kupelekwa Belize, nchi iliyoko Amerika ya Kati.

Gereza la Guantanamo, linalotambulika kama mahabusu inayosifika kwa ubaya zaidi duniani, ambalo kwa miaka 21 sasa linafanya kazi ya kushikilia watu wanaowekwa kizuizini na utawala wa Marekani, limekuwa nembo ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa katika mihula ya marais wanne wa Marekani George W. Bush, Barack Obama, Donald Trump na hivi sasa Joe Biden. Gereza hilo la kuogofya ambalo lilifunguliwa mwaka 2002 na kuwekwa ndani yake wafungwa 780 kutoka nchi 48 lingali linaendelea kushikilia watu hadi sasa.

Kwa mujibu shirika la habari la IRNA, maafisa wa Marekani wamedai kuwa Khan, ambaye sasa ana umri wa miaka 42, alikiri makosa mwaka 2012 ya kula njama na wanachama wa mtandao wa al-Qaeda, ambao walidai kuhusika na mashambulizi ya 2001, na tangu wakati huo amekuwa Guantanamo Bay kama shahidi wa serikali ya Marekani katika kesi hiyo.

Akizungumza baada ya kuachiwa huru, Majid Khan, Khan, ambaye alitekwa nchini Pakistan mwaka 2003 na kupelekwa Guantanamo miaka mitatu baadaye, amesema anatazamia kuanza ukurasa mpya wa maisha yake katika taifa hilo la Amerika ya Kati lenye watu 400,000.

"Leo, ninahisi kama nimezaliwa upya. Nimeingia tena duniani,” ameeleza Muislamu huyo Mpakistan kupitia taarifa aliyotoa.

Ameongeza kuwa, kuachiliwa kwake kumempa mshtuko kidogo kwa sababu amekuwa akingojea kwa muda mrefu kuwa huru, na hawezi kuamini kama hatimaye hilo limetokea.

Ripoti iliyotolewa mwaka 2014 na Seneti ya Marekani ilieleza kwa kina baadhi ya mbinu za mateso zilizotumiwa kwa wafungwa walioko kwenye Gereza la Guantanamo, akiwemo Majid Khan.

"Nilikuwa mzimu, mfu anayetembea," ameeleza Khan katika taarifa yake hiyo na kuongeza kuwa "CIA walitaka nibaki hivi milele. Kwa kweli, nilipokuwa nikiteswa, mara nyingi nilitamani nife ili niepuke hofu na maumivu”.../

342/