Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

4 Februari 2023

11:35:03
1343515

Onyo la Russia kwa Netanyahu kuhusu msaada wa silaha kwa Ukraine

Russia imeuonya vikali utawala haramu wa Israel baada ya Waziri Mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu kutangaza Jumatano usiku kwamba anachunguza suala la kutuma msaada wa kijeshi wa utawala huo nchini Ukraine.

Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, amesema: Kuhusu utoaji wa silaha kwa Ukraine, hatugawanyi pande husika kwa msingi wa jiografia. Tunasema kwamba upande wowote utakaotuma silaha huko Kiev unapasa kujua kwamba tutazichukulia silaha hizo kuwa shabaha ya kushambuliwa kiesheria na vikosi vya Russia.

Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa serikali ya Netanyahu inapitia upya siasa za Tel Aviv kuhusu Ukraine na kuna uwezekano kwa utawala huo kulipatia jeshi la nchi hiyo mifumo ya ulinzi. Eli Cohen, waziri mpya wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni, pia aliihakikishia Ukraine Januari 19 kwamba utawala huo utaendelea kuipa nchi hiyo misaada ya kibinadamu. Inasemekana kuwa Washington imeutaka utawala wa Kizayuni kutuma baadhi ya silaha zake ukiwemo mfumo wa ulinzi wa anga wa Hawk huko Ukraine. Tel Aviv ilinunua mfumo huo kutoka Marekani katika miaka ya sitini.

Takriban muongo mmoja uliopita, jeshi la Israel lilisimamisha matumizi ya mifumo ya Hawk na sasa inatumia mifumo ya kisasa ziadi ambayo inarusha mamia ya makombora kwa wakati mmoja. Pia, gazeti la New York Times liliripoti mwezi uliopita kwamba jeshi la Marekani linatuma kwa siri mamia ya maelfu ya makombora huko Ukraine kutoka kwenye ghala lake kubwa la silaha huko Israel. Kuhusu hilo Netanyahu aliiambia CNN kwamba uamuzi huo ni wa Marekani na kwamba yeye mwenyewe "hana tatizo" na uamuzi huo.

Onyo jipya la Moscow kwa utawala wa Kizayuni linatokana na misimamo na hatua za Tel Aviv kuhusiana na vita vya Ukraine. Russia tayari imeuonya wazi wazi utawala wa Kizayuni kwamba iwapo utatuma huko Ukraine mifumo ya ulinzi wa anga, hata kupitia nchi ya tatu, suala hilo litachukuliwa kuwa ni kuvuka mstari mwekundu na litakuwa na matokeo yake. Moscow imeiambia Tel Aviv kwamba ikiwa makombora ya ulinzi wa anga au makombora mengine yoyote yaliyotengenezwa na utawala huo yatatumwa Ukraine moja kwa moja au kupitia nchi ya tatu, Moscow itatoa jibu kali kwa hatua hiyo.

Hii ni katika hali ambayo utawala wa Israel tayari umeshatuma silaha huko Ukraine. Kwa mujibu wa ripoti za kuaminika, shirika moja la Israel linalohusika na masuala ya kiusalama na uuzaji wa silaha tayari limekwepa marufuku iliyowekwa dhidi ya utawala huo ya kuiuzia Ukraine silaha na kuiuzia mifumo ya makombora ya kutungua ndege zisizo na rubani (drone) kupitia Poland.

Dmitry Medvedev, naibu mkuu wa Baraza la Usalama la Russia ameionya Israel kuhusu kutuma silaha huko Ukraine na kusema: Iwapo hatua hii itatekelezwa, itakuwa ni kitendo cha uzembe na bila shaka kitaharibu uhusiano wa pande mbili.

Uhusiano wa Russia na utawala wa Kizayuni umeingia katika kipindi kipya cha mvutano kufuatia mashambulizi ya Russia huko Ukraine ambapo Tel Aviv imeamua kushirikiana na nchi za Magharibi na kuchukua misimamo ya kiadui dhidi ya Russia. Ingawa mwanzoni mwa vita vya Ukraine, utawala wa Kizayuni ulijifanya kuwa na msimamo usioegemea upande wowote na hata kuzitaka Russia na Ukraine kukubali suluhisho la kisiasa na kusimamisha vita, lakini kufuatia kupanuka wigo wa vita huko Ukraine ambapo Wamagharibi wakiongozwa na Merikani waliamua kuingia moja kwa moja kwenye vita hivyo kwa maslahi ya Kiev, watawala wa Tel Aviv pia waliamua kushirikiana na nchi za Magharibi dhidi ya Moscow.

Watawala hao akiwemo Yair Lapid, waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Israel, waliilaani Moscow kwa madai ya kufanya uhalifu wa kivita nchini Ukraine, na hata Tel Aviv ikaanza kutuma zana za kijeshi kwa jeshi la Ukraine. Hatua ya Israeli kutoa msaada wa kijeshi kwa Ukraine zimefichua zaidi msimamo halisi wa Tel Aviv kuhusu mzozo huo. Kutokana na Israel kupuuza maonyo ya Russia kuhusu vita vya Ukraine, Moscow, katika hatua ambayo ilikuwa haijawahi kushuhudiwa tena huko nyuma, imeamua kupiga marufuku nchini Russia shughuli za shirika moja la Kiyahudi ambalo linahesabiwa kuwa moja ya asasi muhimu zaidi za Wazayuni huko Russia, shirika ambalo limehusika pakubwa katika kuwahamishia Wayahudi wenye asili ya Russia huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kufuatia kuundwa serikali mpya ya Netanyahu, siasa za utawala wa Kizayuni kuhusu vita vya Ukraine sasa zinazingatiwa na kufuatiliwa kwa karibu katika ngazi za kimataifa. Netanyahu anakabiliwa na mashinikizo makubwa kutoka Marekani na Ukraine kwa ajili ya kutuma nchini humo mifumo ya ulinzi wa anga. Kutimizwa matakwa hayo bila shaka kutaibua hisia kali kutoka Moscow na huenda kukaifanya Russia kutazama upya uhusiano wake na utawala huo wa Kizayuni. Onyo kali la karibuni la Zakharova kwa Tel Aviv linaweza kutathminiwa kama ishara ya mambo yanayokuja katika uwanja huo.


342/