Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

4 Februari 2023

11:36:22
1343518

Iran yajibu uropokaji wa Macron, yamtaka azungumzie silaha za nyuklia za Israel

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa matamshi ghalati ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa aliyedai katika mazungumzo yake na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel kuwa, eti Paris inatiwa wasiwasi na shughuli za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu.

Nasser Kan’ani jana Ijumaa alijibu bwabwaja hizo za Macron, ambapo amemtaka rais huyo wa Ufaransa azungumzie silaha za nyuklia zinazomilikiwa na Israel kinyume cha sheria, badala ya kushughulishwa na miradi ya amani ya nyuklia ya Iran.

Macron juzi Alkhamisi alidai kuwa, hakuna shaka kuwa, shughuli za nyuklia za Iran zitakabiliwa na matokeo mabaya. Macron alisema hayo siku moja baada ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kuituhumu Iran kwa kufanya mabadiliko ambayo hayajatangazwa kwenye muunganisho kati ya makundi mawili ya mashine za hali ya juu zinazorutubisha madini ya urani hadi kufikia kiwango cha asilimia 60 katika kituo chake cha Fordow.

Kan'ani amejibu uropojaki huo wa Macron kwa kusema, badala ya kuzungumzia miradi ya nyuklia yenye malengo ya kiraia ya Iran, rais wa Ufaransa angepasa kujadili makumi ya vichwa kwa mabomu ya atomiki vinavyomilikiwa na utawala wa Kizayuni, huku utawala huo ukikataa kufanyiwa ukaguzi na taasisi za kimataifa kama IAEA.

Iran siku ya Alkhamisi ililalamikia ripoti hiyo ya Jumatano ya IAEA kuhusu shughuli za nyuklia za kituo cha nyuklia cha Fordow hapa nchini na kusema, tafsiri ya mkaguzi wa IAEA aliyetembelea kituo hicho cha nyuklia haikuwa sahihi.

Ikumbukwe kuwa, Novemba 2022, Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA alisema shirika hilo halina ushahidi wowote wa kuthibitisha kuwa Iran ina lengo na shabaha ya kumiliki silaha za nyuklia.

Kan'ani ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni ambao una rekodi nyeusi ya uvamizi wa kijeshi na kukalia kwa mabavu ardhi (za Wapalestina na miinuko ya Golan ya Syria), ndio tishio kuu kwa amani na usalama wa eneo na kimataifa.

342/