Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

4 Februari 2023

11:37:19
1343520

Malengo ya safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia nchini Iraq

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al-Saud, tarehe Pili Februari alitembelea Iraq. Safari hiyo ya Bin Farhan inaweza kutathminiwa katika kalibu ya masuala ya kikanda na kimataifa.

Katika ngazi ya ndani, Iraq na Saudi Arabia zinafanya jitihada za kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili. Iraq, ambayo matatizo yake ya kiuchumi yanatambuliwa kuwa kisigino cha Achilles, inataka Saudi Arabia iwekeze katika nchi hiyo, na wakati huo huo Saudia inajaribu kuongeza ushawishi wake katika nchi hiyo kupitia njia ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na Iraq. Suala hili limesisitizwa katika kikao cha juzi cha Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia na Spika wa Bunge la Iraq. Katika mkutano huu, pande hizo mbili zilijadili mahusiano baina ya nchi na njia za kupanua ushirikiano katika sekta ya uchumi, uwekezaji na uratibu wa pamoja kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa. Spika wa Bunge la Iraq, Mohammed al-Halbousi amesisitiza umuhimu wa kuanzishwa tena Baraza la Uratibu la Iraq na Saudia na kamati nyingine za pamoja na kusema kuwa Bunge la Iraq linaunga mkono hatua za serikali za kuimarisha uhusiano wa pande mbili na liko tayari kuondoa vikwazo vya kisheria vinavyohusiana na upanuzi wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Kwa upande wake, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia amesema viongozi wa nchi hiyo wanakaribisha suala la kuimarishwa uhusiano na Iraq katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na uwekezaji ili Iraq iwe na uchumi thabiti.

Katika ngazi ya kikanda, katika miaka ya hivi karibuni, Saudi Arabia imetilia mkazo suala la kustawishwa uhusiano wake wa nje na nchi nyingine za eneo hili la Magharibi mwa Asia na kupunguza mivutano katika siasa za nje. Katika suala hili, mvutano wa miaka 3 na nusu wa Saudia na Qatar ulimalizwa mnamo Januari 2021 na pande hizo mbili sasa zimehuisha tena mahusiano yao. Vilevile, Riyadh imekaribisha mazungumzo ya kusitisha mapigano nchini Yemen; na ingawa mazungumzo haya bado hayajazaa matunda, lakini mashambulizi ya Saudia dhidi ya Yemen yamepungua.

Miongoni mwa matukio muhimu katika siasa za kigeni za Saudi Arabia ni mazungumzo nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia. Uhusiano kati ya Tehran na Riyadh ulikatwa tangu 2016. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, duru 5 za mazungumzo kati ya maafisa wa nchi hizo mbili zimefanyika huko Baghdad kwa upatanishi wa Iraq, na katika miezi ya hivi karibuni maafisa wa Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametangaza mara kwa mara utayarifu wao wa kuendelea na mazungumzo na kuboresha mahusiano.

Inaonekana kuwa moja ya malengo makuu ya safari ya Faisal bin Farhan Al-Saud huko Baghdad ni kujadili suala la kuendelezwa mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kabla ya hapo, Fuad Mohammed Hussein Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq alitangaza safari tarajiwa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia mjini Baghdad ili kuanzisha tena mazungumzo kati ya Tehran na Riyadh.

Suala hili pia lina umuhimu mkubwa kwa serikali ya Iraq. Kwa upande mmoja, Iraq inataka kuwa na nafasi katika matukio ya kikanda, na hapana shaka kuwa kuandaa mazungumzo ya Iran na Saudia ni moja ya masuala muhimu yanayoweza kutimiza lengo hilo la Iraq. Katika upande mwingine, Iraq sawa na nchi nyingine za eneo hili, inafahamu vyema kwamba, kuboreka uhusiano kati ya Tehran na Riyadh kuna taathira muhimu si tu kwa nchi hizo bali pia kwa nchi nyingine na eneo la Magharibi mwa Asia na katika kupunguza mvutano na machafuko katika eneo hilo.

342/