Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

3 Februari 2024

19:33:51
1434890

Hizbullah: Njia pekee ya kuondoa wasiwasi ni kukomeshwa mauaji ya kimbari Ghaza

Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, harakati hiyo imejiweka tayari kukabiliana na vitisho vyovyote vya utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa, njia pekee ya kuondoa wasiwasi uliopo ni Israel kukomesha mauaji ya watu wasio na hatia huko Ghaza, Palestina.

Sheikh Naim Qassim alisema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, Lebanon ilitangaza uungaji mkono wake kwa wananchi wa Ghaza mara baada ya utawala wa Kizayuni kuanzisha mashambulizi dhidi ya wakazi wa ukanda huo na uungaji mkono huo utaendelea hadi pale Israel itakapokomesha jinai zake dhidi ya raia wa Ghaza.

Kwa upande wake, Sheikh Nabil Qawuq, mjumbe wa Kamati Kuu ya Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, muqawama nchini Lebanon uumejiandaa kikamilifu kwa ajili ya kukabiliana na hali yoyote ile.

Amesema, muqawama unaonesha nguvu zake kwenye medani za mapambano na kwamba vitisho vya maneno vya Wazayuni haviwezi kubadilisha chochote. Amesema, kadiri utawala wa Kizayuni unavyotanua wigo wa mashamblizi yake nchini Lebanon ndivyo unavyozidi kupata kipigo kwani muqawama hauchelewi hata kidogo kujibu vikali hujuma zozote za Wazayuni. Siku 120 zimepita tangu utawala wa Kizayuni wa Israel uanze kufanya mauaji ya umati kwenye Ukanda wa Ghaza huko Palestina na hadi hivi sasa zaidi ya Wapalestina 27,000 wameshauawa shahidi wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake. Makumi ya maelfu ya Wapalestina wengine wamejeruhiwa na wengine hawajulikani walipo. Katika kipindi chote hicho cha jinai za Israel huko Ghaza, makundi ya muqawama ya Palestina, Lebanon, Yemen na Iraq nayo yamekuwa yakifanya mashambulizi ya kujibu jinai za utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake katika maeneo tofauti ya Palestina, Iraq, Syria na Yemen.

342/