Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

12 Februari 2024

19:27:09
1437184

Mahakama ya Uholanzi yaiamuru Serikali isimamishe kuipatia Israel vifaa vya ndege za kivita

Mahakama ya Uholanzi imeiamuru serikali kusitisha utoaji wa vifaa na vipuri vya ndege za kivita za F-35 zinazotumiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika mashambulizi yake ya kinyama unayofanya katika Ukanda wa Gaza.

Amri hiyo imetolewa kufuatia rufaa iliyokatwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Oxfam dhidi ya uamuzi wa mahakama ya chini uliokataa hoja yao kwamba utoaji wa vifaa hivyo unachangia ukiukaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na Israel.

Mwaka jana, matawi ya mashirika ya haki za binadamu nchini Uholanzi yaliishutumu serikali ya nchi hiyo kwa kuhusika katika uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa na utawala wa Kizayuni wakati wa vita vyake huko Gaza kutokana na kuuuzia utawala huo vifaa vya ndege za kivita za F-35.

Matawi ya Amnesty International na Oxfam nchini Uholanzi yalisema katika mashtaka yao kwamba shehena hizo "zinachangia kwa kiasi kikubwa ukiukaji mkubwa wa sheria za kibinadamu unaofanywa na Israel huko Gaza".

Lakini mnamo mwezi Desemba, mahakama ilitupilia mbali kesi hiyo na kusema kuwa serikali lazima ipewe uhuru mkubwa wakati wa kuamua juu ya masuala ya kisiasa na kisera kuhusu uuzaji wa silaha nje ya nchi.

Hata hivyo katika uamuzi uliotangazwa leo, mahakama ya rufaa imeiamuru serikali ya Uholanzi kusimamisha ndani ya siku saba usafirishaji wote wa vifaa vya ndege za kivita kwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

"Ni jambo lisilopingika kwamba, kuna hatari ya wazi ya vipuri vya F-35 vinavyosafirishwa nje kutumika katika ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu," alisema Jaji Bas Boele wakati akisoma uamuzi huo, na kuibua shangwe kutoka kwa watu kadhaa katika chumba cha mahakama.

Mahakama hiyo imeongeza kuwa kuna uwezekano kwamba vifaa hivyo vitakuwa vinatumika katika mashambulizi huko Gaza, na kusababisha idadi kubwa ya vifo vya raia.

Hayo yanajiri huku Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza ikitangaza leo kuwa, Wapalestina wapatao 28,340 wameuawa shahidi katika eneo hilo lililozingirwa wakati wote wa vita, ikiwa ni pamoja na 164 waliouliwa katika saa 24 zilizopita. Jumla ya Wapalestina 67,984 wamejeruhiwa tangu utawala katili wa Kizayuni wa Israel ulipoanzisha mashambulio ya kinyama dhidi ya Gaza Oktoba 7, 2023.../

342/