Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

19 Februari 2024

19:14:20
1439067

Iran: Kuipatia Israel dola bilioni 14 ni sawa na Marekani kutoa bakhshishi kwa mauaji ya Wapalestina

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, kuidhinishwa na Baraza la Seneti la Marekani msaada wa dola bilioni 14 kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kunaonyesha kuwa Washington inautuza na kuupa bakhshishi utawala huo kwa kuwaua kwa halaiki raia wasio na hatia wa Palestina katika vita visivyo na mlingano vya Gaza.

Nasser Kan'ani ameeleza katika ujumbe alioweka kwenye ukurasa wa kijamii wa X kwamba fungu la fedha lililoidhinishwa na Marekani, kwa kuchangiwa na walipa kodi wa nchi hiyo linaonyesha kwamba watu kama waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu pamoja na wauaji wenzake wengine katika vita vya Gaza, "watazawadiwa kila siku kiasi cha dola milioni mia moja kutoka Marekani kwa mauaji ya raia wasio na hatia wa Palestina." 

Kan'ani ameongeza kuwa, ni tawala za kifisadi na za kidhalimu pekee, zilizojikita katika kutoa roho za watu, ndizo zinazoweza kufuja fedha kwa ajili ya mauaji ya watu wasio na hatia.

Baraza la Seneti la Marekani Jumanne iliyopita lilipitisha fungu la msaada wa dola bilioni 95.34 kwa ajili ya Ukraine, Israel na Taiwan.

Mgao wa fungu hilo la fedha unajumuisha dola bilioni 61 kwa ajili ya Ukraine, dola bilioni 14 kwa ajili ya utawala wa Kizayuni wa Israel na dola bilioni 4.83 kusaidia mhimili unaopinga China katika eneo la Indo-Pasifiki, hususan kisiwa cha Taiwan.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hadi sasa zaidi ya Wapalestina 28,985, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa shahidi na wengine zaidi ya 68,880 wamejeruhiwa tangu utawala haramu wa Israel ulipoanzisha mashambulizi ya kikatili na mauaji ya kinyama yanayoungwa mkono kwa kila hali na Marekani dhidi ya Gaza Oktoba 7, 2023.../

342/