Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

23 Februari 2024

16:26:20
1439815

Ukosoaji wa Qatar dhidi ya Israel; Rekodi mpya ya waandishi wa habari waliouawa Gaza

Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Qatar, Lolwah Al-Khater, ameeleza masikitiko yake kwamba: Israel imeweka rekodi ya kushambulia na kuua waandishi wa habari.

Mwezi wa tano wa vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza unaelekea ukingoni. Vita hivi vimeandamana na mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza. Waandishi wa habari ni miongoni mwa makundi ambayo yamekuwa yakilengwa kwa ukatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala huo umeua waandishi wa habari 127 katika kipindi cha miezi mitano iliyopita ya mashambulizi yake huko Gaza.

Takwimu zinaonyesha kuwa, Israel imekuwa ukimuua shahidi mwandishi mmoja wa habari wa Kipalestina takriban kila siku. Mashambulizi ya Israel dhidi ya waandishi na wawakilishi wa vyombo vya habari yalianza tangu siku za kwanza kabisa za uvamizi wa jeshi la utawala huo huko Gaza. 

Kwa mujibu wa ripoti ya mashirika ya kimataifa, katika mwezi wa kwanza wa mashambulio ya Wazayuni huko Gaza, waandishi wa habari wasiopungua 39 waliuawa, idadi ambayo ni zaidi ya mara mbili ya waandishi habari waliopoteza maisha katika vita vya mwaka mmoja na nusu kati ya Russia na Ukraine; Kwa sababu hiyo, kipindi hicho kilipewa jina la "mwezi mbaya zaidi kwa waandishi wa habari" katika mwaka 2023.

Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari pia iliripoti kwamba "idadi ya waandishi wa habari waliouawa katika mwezi wa kwanza wa vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza ilikuwa kubwa zaidi kuliko idadi ya waandishi habari waliouawa katika mgogoro mwingine wowote katika mwezi wa kwanza wa vita, tangu kuanza kazi kamati hii mwaka 1992."

Anthony Bellanger, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari, ameviambia vyombo vya habari vya kimataifa kwamba: "Naweza kusema kwamba katika vita kama vya Syria, Iraqi na Yugoslavia ya zamani hatujaona mauaji ya aina hii ya waandishi wa habari kama ilivyotokea huko Gaza."

Uhalifu dhidi ya waandishi wa habari unatambuliwa kuwa jinai ya kivita kwa mujibu wa sheria za kimataifa, na kuwalenga kwa makusudi waandishi wa habari na raia kumetajwa kuwa ni uhalifu wa kivita. Vilevile sheria hizo zinasisitiza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuruhusiwa kufanya kazi kwa uhuru na kupewa ulinzi wa kutekeleza majukumu yao bila kuingiliwa isivyostahili katika mizozo yote. 

Suala na nukta nyingine ni kwamba, jamii ya kimataifa, mbali na kukaa kimya dhidi ya mauaji yanayofanywa na utawala ghasibu wa Israel huko Ghaza, imepuuza mauaji ya Israel dhidi ya waandishi wa habari ambao hawana jukumu lolote katika vita na mapigano hayo isipokuwa kuwanukulia walimwengu picha na habari za yanayojiri.

Katika mkondo huo, Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Qatar, Lolwah Al-Khater, ameyataja mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Gaza kuwa ni "mauaji ya kimbari ya watoto" na kusema: Vita vya Gaza vimefichua unafiki na sera za kindumakuwili za Magharibi kwa ulimwengu wote. Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Qatar ameongeza kuwa: Jeshi la Israel limekiuka sheria zote za haki za binadamu za mikataba na hati za Umoja wa Mataifa.