Main Title

source : Parstoday
Jumapili

28 Aprili 2024

20:10:29
1454812

Mjukuu wa Mandela: Afrika Kusini imepata msukumo kutokana na uthabiti wa Wapalestina

Mjukuu wa Nelson Mandela amesema Afrika Kusini imetiwa moyo na kupata msukumo kutokana na istikama na uthabiti wa Wapalestina; na kwa sababu hiyo ikaileta hoja ya piganio lao mbele ya Jamii ya Kimataifa.

Nkosi Zwelivelile Mandela, ambaye ni mbunge katika Bunge la Afrika Kusini ameyasema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la Anadolu mjini Istanbul na kufafanua kwa kusema: "tunazidi kuhamasishwa na uthabiti wa Wapalestina na kwa hakika hatutawakatisha tamaa katika kufikisha simulizi zao na fahari yao kwa jamii ya kimataifa".  Afrika Kusini ilikuwa nchi ya kwanza kuiomba Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) iutie hatiani utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza. Uamuzi wa muda uliotolewa mwezi Januari na mahakama hiyo uliuamuru utawala huo ghasibu usitishe vitendo vya mauaji ya kimbari na kuchukua hatua za kuhakikisha msaada wa kibinadamu unawafikia raia huko Ghaza.
Mandela amesisitiza kwa kusema: "bila shaka, kwetu sisi Waafrika Kusini, suala la Palestina daima limekuwa karibu nasi na muhimu sana mioyoni mwetu. Baba mwanzilishi wa demokrasia ya taifa letu, Mheshimiwa Rais Nelson Mandela, ambaye ni babu yangu, alipotembelea Ghaza mwaka 1995, na mwaka 1997 alisema na kutoa ahadi kwa Wapalestina kwamba uhuru wetu haujakamilika bila uhuru wa watu wa Palestina". Akiwa mjumbe wa taasisi ya kimataifa ya Global Return Campaign of Global Palestine inayotetea na kuunga mkono piganio la Palestina katika ulimwengu wa Kiarabu na kimataifa kwa Wapalestina kurudi kwenye ardhi zao za asili, Mandela amezungumzia pia kesi zilizofunguliwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na kueleza kwamba, kwa mara ya kwanza Afrika Kusini kama nchi imeweza kuuwajibisha utawala ghasibu wa Kizayuni baada ya kipindi cha miaka 76 kwa mauaji ya kimbari, uangamizaji wa kizazi, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu unaofanya. Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Nkosi Zwelivelile Mandela amesisitizia haja ya kufanyika "mageuzi" katika taasisi za kimataifa hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na umoja huo pia. Amesema: "tumeona mara kwa mara, hoja inapoletwa ndani ya Umoja wa Mataifa inapingwa kwa kura ya veto na nchi moja mwanachama ambayo huwezesha wahalifu kuendeleza mauaji ya kimbari, uangamizaji wa kizazi, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu".../

342/