Main Title

source : Parstoday
Jumatano

15 Mei 2024

17:15:19
1458818

IDMC: Kuna ongezeko kubwa la ukimbizi wa ndani unaosababishwa na migogoro duniani

Ripoti mpya ya Kituo cha Ufuatiliaji wa Ukimbizi wa Ndani (IDMC) inaonyesha kuwa migogoro na ghasia duniani zimesababisha ongezeko lisilo na kifani la idadi ya wakimbizi wa ndani kufikia mwisho wa 2023.

Gazeti la Guardian linalochapishwa London nchini Uingereza, limenukuu taarifa ya Kituo cha Ufuatiliaji wa Ukimbizi wa Ndani (IDMC) chenye uhusiano na Baraza la Wakimbizi la Norway, na kuandika kwamba, ripoti mpya ya kituo hicho inaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka jana 2023, migogoro katika nchi tofauti iliwalazimisha zaidi ya watu milioni 68 kuacha nyumba zao na kuwa wakimbizi.

Ripoti ya IDMC inaonyesha kuwa, mipigano ya Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na vita vya mauaji ya kimbari ya Israel katika Ukanda wa Gaza vimesababisha ongezeko la idadi ya wakimbizi wa ndani duniani kote.

Takwimu za kituo hicho zinaonyesha kuwa, majanga ya kimaumbile yamewafanya watu wengine milioni 7.7 kukosa makazi na idadi ya wakimbizi wa ndani imefikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa cha watu milioni 75.9. Ripoti hiyo inasema, ongezeko la idadi ya wakimbizi duniani ni matokeo ya vita na migogoro mipya na ya zamani ambayo imewafanya watu washindwe kurejea katika nchi zao. IDMC inasema, katika nchi za Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, idadi ya wakimbizi wa ndani imeongezeka zaidi ya mara mbili kutoka watu milioni 16.5 mwaka 2018 hadi watu milioni 34.8 mwishoni mwa 2023. Sudan inachangia asilimia 45 ya wakimbizi katika eneo hilo, ikifuatiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

342/