Main Title

source : Parstoday
Jumanne

28 Mei 2024

16:53:37
1461894

Kaimu Rais wa Iran asisitiza kuhusu kuimarishwa uhusiano wa kibiashara wa Iran na Oman

Kaimu Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja uhusiano wa Iran na Oman kuwa wa kihistoria na wa kidugu na kusema: Iwapo uwezo uliopo utatumika vizuri, maingiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya Iran na Oman yataongezeka hadi mara kadhaa ya kiwango cha sasa.

Mohammed Mokhber, Kaimu Rais wa Iran, Jumatatu alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Badr bin Hamad al-Busaidi, ambapo ameishukuru kwa dhati serikali na watu wa Oman kwa kutuma salamu za rambirambi na kufungamana na Iran baada ya kufa shahidi Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Iran na Waziri wa Mashauri ya Kigeni Hossein Amir-Abdollahian. Mokhber amesisitiza kuendelea stratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuendeleza na kupanua ushirikiano wa pande zote na Oman.

Huku akiutaja uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman kuwa wa kihistoria na wa kidugu, Mokhber amesema: "Kuna uwezo ambao haujatumika katika nchi hizi mbili hususan katika sekta ya uchumi."

Badr bin Hamad al-Busaidi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Oman pia ameeleza kuwa amekuja Iran na salamu za rambirambi za Sultan Haitham bin Tariq, serikali na taifa la Oman kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran.

Ameongeza kuwa, taifa la Oman limepoteza marafiki zake wa karibu katika tukio hilo chungu na la kusikitisha na kuwa liko pamoja na taifa la Iran katika wakati huu wa majonzi.

Ameitakia mafanikio serikali ya Iran katika kuendelea kulitumikia taifa, na vile vile kutimiza malengo ya rais aliyekufa shahidi katika kuendeleza na kufanya maingiliano na nchi za Kiislamu ikiwemo Oman. Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman pia ameutaja uhusiano kati ya Iran na Oman kuwa ni wa kistratijia na muhimu, na akaeleza nia ya nchi yake ya kuimarisha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

342/