Main Title

source : Parstoday
Jumatano

29 Mei 2024

20:53:35
1462128

Ripoti: Chuki dhidi ya Waislamu Austria zimefikia kiwango cha juu

Austria imerekodi idadi kubwa zaidi ya matukio ya chuki dhidi ya Uislamu katika mwaka uliopita wa 2023 tangu ilipoanza kuweka rekodi za matukio hayo mwaka 2015.

Ripoti ya kila mwaka ya Kituo cha Nyaraka kuhusu chuki dhidi ya Uislamu na Ubaguzi dhidi ya Waislamu imesema, idadi ya kesi zilizoripotiwa imeongezeka, hususan tangu vilipoanza vita vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza mnamo Oktoba 7 mwaka jana. Kesi nyingi zaidi zilirekodiwa kuanzia Oktoba hadi Desemba kuliko katika miezi tisa ya kwanza ya 2023. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mahali pa kwanza paliporipotiwa kesi nyingi zaidi kuanzia mwezi Oktoba ni mashuleni. Katika sekta ya elimu, matukio ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu yameripotiwa na wazazi, wanafunzi na walimu. Kwa jumla, 66.7% ya kesi zilizorekodiwa zilifanyika kwenye mitandao ya kijamii na 33.7% nje ya mitandao hiyo. Takriban 87.8% ya visa vilivyorekodiwa mtandaoni vilihusu uenezaji chuki.Ripoti ya Kituo cha Nyaraka kuhusu chuki dhidi ya Uislamu na Ubaguzi dhidi ya Waislamu nchini Austria imeendelea kubainisha kuwa Waislamu wamedunishwa na kuvuliwa utu wao kwa kulinganishwa na wanyama katika maoni mbalimbali ya hisia za chuki yaliyotolewa mitandaoni.

Watu wengi waliotoa maoni hayo ya chuki waliwahusisha Waislamu peke yao na tuhuma za kueneza chuki dhidi ya Wayahudi.

Katika ripoti yake hiyo, kituo hicho cha nyaraka cha Austria kimesisitiza kuwa takwimu ilizotoa ni muhtasari tu wa matukio, lakini idadi halisi ya kesi hizo inaaminika kuwa kubwa zaidi.

Ripoti hiyo imemalizia kwa kutoa indhari kwamba takwimu hizo "ni hali ya kutia wasiwasi" juu ya mambo yanayochangia zaidi mgawanyiko na mpasuko katika jamii na kutaka kushughulikiwa kwa umakini zaidi tatizo la uenezaji chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.../

342/