Main Title

source : Parstoday
Jumatano

29 Mei 2024

20:58:55
1462139

Trump aapa "kutimua wanafunzi" na kukandamiza wanaounga mkono Palestina akichagualiwa tena kuwa rais

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ameapa kuwa atakandamiza maandamano ya watetezi na waungaji mkono wa Palestina yanayoendelea kufanywa katika vyuo vikuu vya nchi hiyo na kusisitiza kuwa "atawafukuza" wanafunzi wanaohudhuria maandamano hayo, ikiwa atachaguliwa kurudi tena madarakani.

Akizungumza kwenye hafla iliyoandaliwa na kikundi kidogo cha wafadhili ambao wengi wao ni Wayahudi, Trump amesema, atawafukuza waandamanaji wote wanaounga mkono Palestina ili kuhakikisha kuwa "wanajiheshimu." Rais huyo wa zamani wa Marekani amelifafanua hilo kwa kusema: "jambo moja nitakalofanya ni kwamba, mwanafunzi yeyote atakayeandamana nitamfukuza nchini. Unajua, kuna wanafunzi wengi wa kigeni. Mara tu watakaposikia hivyo, watajihesimu". Trump, mwenye umri wa miaka 77, ambaye anatarajiwa kuwa ndiye atakayegombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican, ameyaelezea maandamano ya kupinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ghaza kuwa ni "mapinduzi hatari" na kuwahakikishia wafadhili hao kwamba, kwa msaada na uungaji mkono wao, atalirudisha miaka 25 au 30 nyuma vuguvugu hilo kwa kumshinda Joe Biden katika uchaguzi ujao wa rais utakaofanyika mwezi Novemba.Katika miezi ya hivi karibuni, maandamano ya kupinga jinai za kinyama za mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza yametikisa taasisi mbalimbali za elimu katika kila pembe ya Marekani. Harakati hizo zilianzia Chuo Kikuu cha Columbia mjini New York, ambapo uwekaji mahema na kupiga kambi kwenye viwanja vya vyuo kulivuruga shughuli za masomo katika wiki za mwisho na kupelekea hata kuakhirishwa mahafali za kuhitimu masomo.

Kwa mujibu wa gazeti la The Washington Post, wafadhili wa chama cha Republican wamemtaka Trump achukue msimamo mkali zaidi wa kuiunga mkono Israel na waziri mkuu wake Benjamin Netanyahu.

Trump pia ameripotiwa kuwaambia wafadhili hao katika faragha kwamba anaunga mkono haki ya utawala huo wa Kizayuni ya kuendeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza.../


342/