Main Title

source : Parstoday
Jumatano

29 Mei 2024

21:01:29
1462140

Licha ya amri ya ICJ Israel yaongeza brigedi nyingine ya kijeshi, mbali na 5 zilizoko Rafah

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limetangaza kuwa linatuma kikosi kingine cha mapigano huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Ghaza, kujiunga na brigedi tano ambazo tayari ziko katika mji huo, huku jeshi hilo likipanua wigo wa uvamizi wake katika mji huo.

Kwa mujibu wa Redio ya Jeshi la Israel, kikosi cha jeshi cha brigedi ya Biislamach kiliingia Rafah siku ya Jumatatu, na kuwa kikosi cha sita cha mapigano cha jeshi la Kizayuni kupelekwa katika mji huo. Redio hiyo imelielezea tangazo hilo kama kielelezo cha kupanuliwa kivitendo operesheni ya uvamizi ya jeshi la Israel huko Rafah iliyoanzishwa tarehe 6 ya mwezi huu wa Mei. Kutumwa kikosi kipya cha mapigano mjini Rafah kunafanyika licha ya amri iliyotolewa Ijumaa iliyopita na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ya kuutaka utawala wa Kizayuni usitishe mara moja mashambulizi yake katika mji huo uliofurika Wapalestina waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulio ya jeshi la utawala huo.Upanuzi wa sasa wa operesheni ya kuivamia kijeshi Rafah unalifanya jeshi la Kizayuni likaribie kulidhibiti kikamilifu eneo la mpaka kati ya Ukanda wa Ghaza na Misri, linalojulikana kama Ukanda wa Philadelphia.

 Jeshi la Israel hadi sasa limedhibiti karibu theluthi mbili ya eneo la ukanda huo huku likiendelea kusonga mbele kwa kufanya mashambulizi makali ya mabomu na makombora. Utawala haramu wa Kizayuni unaendeleza mashambulizi yake ya kikatili huko Ghaza licha ya azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka kusitishwa mara moja mapigano katika eneo hilo lililowekewa mzingiro. Wapalestina wapatao 36,050 wameshauawa shahidi huko Ghaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na wengine zaidi ya 81,000 wamejeruhiwa tangu jeshi la Kizayuni lilipoanzisha mashambulio ya kinyama ya mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo Oktoba 7, 2023.../

342/