Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

7 Juni 2024

15:11:35
1463970

Iran yazitaka nchi za Waislamu kuunganisha nguvu zao kukabiliana na Israel

Katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitizia ulazima wa kuunganishwa nguvu za nchi za Waislamu katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni.

Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kumnukuu Ali Bagheri, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisema katika mazungumzo ya simu ya jana Alkhamisi na Sameh Shukri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, kwamba,  jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza na uvamizi wake kwenye mji wa Rafah, unazilazimisha nchi za Waislamu kutumia uwezo wao wote ikiwa ni pamoja na uwezo wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, kukomesha mauaji ya kimbari ya Wazayuni huko Ghaza na kuongeza kasi ya kutumwa misaada ya kimataifa ya kibinadamu katika ukanda huo.

Aidha Bagheri ametumia fursa hiyo kutoa shukurani zake kwa serikali ya Misri kwa kutuma rambirambi zake kwa Jamhuri ya Kiislamu baada ya kufa shahidi Rais wa Iran Sayyid Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Amir-Abdollahian na wenzao sita, kwenye ajali ya helikopta. 

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, ametumia mazungumzo hayo ya siku kusisitiza kuwa nchi mbili za Iran na Misri zina mambo mengi ya kushirikiana na kwamba inabidi fursa hiyo itumiwe vizuri kadiri inavyowezekana. Vile vile amesema kuwa, katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, Cairo imeongeza juhudi zake za kuhakikisha vita dhidi ya Ghaza vinasimamishwa na imetoa ushirikiano wa kutosha katika juhudi za kuhakikisha mazingira ya kupelekwa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Ghaza yanakuwepo.

342/