Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

7 Juni 2024

15:12:22
1463972

Guterres alaani vikali hujuma ya Israel iliyoua wakimbizi 35 katika kituo cha UNRWA Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani shambulio lililofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye shule iliyokuwa inahifadhi wakimbizi wa kipalestina huko Nuiserat, katikati mwa Gaza alfajiri ya Alhamisi.

Amesema shambulio hilo ni mfano mwingine wa gharama wanayolipa raia wanaohaha kusaka usalama.

Stéphane Dujarric ambaye ni msemaji wa Katibu Mkuu amesema hayo alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari jijini New York aliyetaka kufahamu iwapo Guterres ana kauli yoyote kuhusu shambulio hilo lililosababisha vifo vya watu 35 na wengine wengi wamejeruhiwa.

Dujarric amesema, “Nazungumza kwa niaba yake (Guterres). Kwa hiyo naweza kukueleza kwamba amesema shambulio hilo ni mfano mwingine wa kutisha wa gharama wanayolipa raia wa kipalestina, wanaume, wanawake na watoto ambao wanajaribu kuishi, wanaolazimika kukimbia hapa na pale kama mzunguko wa kifo ndani ya Gaza, wakijairbu kusaka usalama.

Alipoulizwa iwapo Katibu Mkuu analaani shambulio hilo kwenye shule hiyo iliyokuwa inahifadhi wakimbizi 6,000, Dujarric amesema, “bila shaka analaani shambulio hili.”

Jeshi la anga la utawala wa Kizayuni wa Israel alfajiri ya kuamkia jana Alhamisi lilishambulia kwa makombora skuli ya Umoja wa Mataifa katika kambi ya Nuseirat katikati mwa Ukanda wa Ghaza na kuwaua shahidi Wapalestina wasiopungua 35 wakiwemo watoto na wanawake na kujeruhi makumi ya wengine.

Maelfu ya Wapalestina waliolazimika kuyahama makazi yao walikuwa wamepatiwa hifadhi katika skuli hiyo ya kambi ya Nuseirat ya al-Sardi, ambayo inasimamiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Mkuu, UNRWA, Philippe Lazarini amesema kushambulia, kulenga au kutumia majengo ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya shughuli za kijeshi ni kinyume na sheria za kimataifa za kibinadamu,