Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

7 Juni 2024

15:14:15
1463976

Uhispania yajiunga na kesi ya Afrika Kusini ICJ dhidi ya Israel

Siku chache baada ya Uhispania kutangaza kulitambua rasmi taifa la Palestina, nchi hiyo ya Ulaya imetuma ombi la kujiunga kwenye kesi ya Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaotenda jinai dhidi ya binadamu huko Gaza.

Akihutubia waandishi wa habari jana Alkhamisi, Jose Manuel Albares, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesema Madrid imechukua uamuzi huo kwa kuwa utawala wa Israel unaendeleza uvamizi wa kijeshi dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Albares amesema Uhispania inatiwa wasi wasi na kupanuka zaidi kieneo mgogoro wa Ukanda wa Gaza. Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Uhispania ameeleza bayana kuwa, nchi yake imefanya maamuzi hayo kwa shabaha ya kurejesha amani si tu katika Ukanda wa Gaza na eneo la Asia Magharibi, lakini pia kutokana na kufungamana kwake na sheria za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesisitiza kuwa, "Lengo hasa la Uhispania la kufanya uamuzi huu (wa kujiunga kwenye kesi ya Afrika Kusini ICJ) ni kuhitimisha vita (Gaza) na kuendeleza njia ya kile kinachoitwa suluhisho la mataifa mawili."

Hadi sasa nchi kadhaa zikiwemo Chile, Mexico, Uturuki, Colombia, Nicaragua na Libya zimeomba kujiunga na kesi hiyo ya Afrika Kusini huko mjini The Hague nchini Uholanzi, kwa ajili ya kuwatetea na kuwaunga mkono Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wanaouawa kila siku na utawala haramu wa Israel.Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez amekuwa mmoja wa viongozi wa Ulaya wanaopinga wazi wazi vita vya mauaji ya halaiki vya utawala wa Israel dhidi ya Gaza.

Amekuwa akisisitiza kuwa, kutambuliwa rasmi Palestina ni haki ya kisheria ya taifa hilo madhulumu na kueleza kwamba, hatua hiyo ilichukuliwa kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa.


342/