Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

7 Juni 2024

15:15:08
1463978

Somalia yachaguliwa kama mjumbe asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Katika upigaji kura uliofanyika kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuchagua wanachama wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama, Somalia imepata uidhinishaji kamili kutoka Afrika na kupata kura 179, zaidi ya theluthi mbili ya wingi unaohitajika kuchaguliwa.

Kwa mara ya mwisho Somalia ilihudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 1971-72, wakati wa utawala wa Siad Barre.

Uidhinishaji huo mpya unamaanisha kuwa Somalia itahudumu katika chombo chenye nguvu zaidi cha Umoja wa Mataifa chenye wanachama 15 kuanzia Januari 2025 hadi Desemba 2026.

Itachukua nafasi ya Msumbiji kama mwakilishi wa Afrika ambaye muhula wake unamalizika Desemba mwaka huu.

Baraza hilo lina wanachama 15 na wanachama watano wa kudumu - Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia - wenye mamlaka ya kura ya turufu katika masuala muhimu.

Wengine 10 kwa kawaida huchaguliwa katika muundo wa mzunguko huku Afrika ikipewa nafasi tatu kwenye Baraza.

Somalia ilichaguliwa bila kupingwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa baada ya Umoja wa Afrika kukubaliana kimsingi kuidhinisha Mogadishu mapema mwaka huu.

Kwa miongo miwili sasa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa likiiwekea Somalia vikwazo kutokana na vita vya ndani nchini humo.

Hata kama Somalia ni mwanachama wa Baraza la Usalama lakini haitaweza kufanya maamuzi kuhusu masuala muhimu kama vile nani aweke vikwazo au vikwazo vipi viondolewe, lakini nafasi hiyo inaipa uwezo kushawishi maamuzi yanayofaa kwa ajili yake na Afrika.

342/