Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

29 Juni 2024

17:14:46
1468526

Uchaguzi wa rais wa Iran waingia duru ya pili, Wairani kupata rais mpya baada ya Ijumaa ijayo

Matokeo rasmi na ya mwisho ya duru ya 14 ya uchaguzi wa rais wa kabla ya wakati wa Iran yanaonesha kuwa zoezi hilo litaingia katika duru ya pili.

Duru hiyo ya pili ya uchaguzi iliyopangwa kufanyika Julai 5, itawachuanisha aliyekuwa Waziri wa Afya na mbunge wa sasa, Masoud Pezeshkian na mkuu wa zamani wa timu ya mazungumzo ya nyuklia, Saeed Jalili. 

Uchaguzi wa 14 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulifanyika jana Ijumaa, Juni 28, 2024 kuanzia saa mbili asubuhi na kuendelea kwa saa 16 baada ya kuongezewa muda mara kadhaa. 

Mohsen Eslami, Msemaji wa Makao Makuu wa Uchaguzi ya Iran amesema baada ya kuhesabiwa kura zote zilizopigwa (24,535,185) kwenye uchaguzi huo wa Ijumaa ya jana Julai 28, Pezeshkian ameibuka kidede kwa kupata kura 10,415,991 huku Jalili akiambulia kura 9,473,298.

Uchaguzi huo umefanyika katika vituo 59,000 vya kupigia kura ndani ya Iran na 95 nje ya nchi. Wairani waliotimiza masharti ya kupiga kura katika uchaguzi huo walikuwa ni milioni 61 na 452,321. 

Wagombea waliochuana kwenye kinyang'anyiro hicho walikuwa ni wanne baada ya wagombea wawili kujitoa. Wachambuzi wa mambo walitabiri mapema kuwa mchuano mkubwa utakuwa ni baina ya Saeed Jalili. Utabiri mwingine wa wachambuzi wa mambo ulikuwa ni kuingia uchaguzi huo katika duru ya pili. Ilitabiriwa pia kuwa mshindi wa tatu katika uchaguzi huo atakuwa ni Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na wa mwisho angelikuwa waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Mostafa Pourmohammadi. Utabiri huo unaonekana umekuwa sawa na ulivyotabiriwa na wataalamu hao baada ya kufanyika uchaguzi huo na kuanza kutangazwa matokea ya kura.Uchaguzi huu wa 14 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umefanyika kabla ya wakati wake kufuatia kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta, tarehe 19 Mei, 2024 kaskazini mwa Iran. 

Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni imara sana kiasi kwamba, licha ya kufariki dunia ghafla Rais Raisi pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian na wenzao kadhaa, lakini nchi haikutetereka kwani kila kitu kimeainishwa katika Katiba. Kwa mujibu wa vifungu nambari 131 na 132  vya Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Makamu wa Kwanza wa Rais, Mohammad Mokhber alishika mara moja nafasi ya kuongoza serikali kwa idhini ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kisilamu ambapo sambamba na kuendesha mambo ya nchi, serikali yake imesimamia pia kufanyika uchaguzi wa jana uliofanyika katika kipindi cha siku 50 tangu kufa shahidi dunia Rais Ebrahim Raisi kama inavyosema Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupiga kura zao humu ndani ya Iran. Wakati wa kupiga kura hiyo, Kiongozi Muadhamu alisema, kujitokeza kwa wingi wananchi katika uchaguzi huo ni jambo la wajibu kwa ajili ya kuutia nguvu mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuuwekea kinga.
Amesema, kujitokeza kwa wingi wananchi wa Iran katika uchaguzi huo kuna ujumbe muhimu wa Jamhuri ya Kislamu kwa marafiki na maadui. Kama lilivyo jina lake yaani Jamhuri ya Kiislamu, mfumo huu wa kiutawala hapa Iran, kwa wakati mmoja ni wa kidini na wakati huo huo ni wa demokrasia kwa maana ya kwamba, maoni ya wananchi nayo yamezingatiwa katika mfumo huu wa demokrasia ya kidini ikiwa ni pamoja na wananchi kutumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi ambao wanaamini wanafaa zaidi kuweza kuwahudumia ndani ya mipaka ya dini tukufu ya Kiislamu. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huchaguliwa kila baada ya miaka minne isipokuwa inapotokezea jambo la dharura kama hili la kufariki dunia rais aliyeko madarakani. Yote hayo yameainishwa na Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa mujibu wa Katiba, Jamhuri ya Kiislamu inaongozwa na mihimili mitatu mikuu yaani Serikali, Bunge na Mahakama. Mkuu wa serikali yaani Rais ndiye mwenye cheo kikubwa zaidi kuliko wakuu wa mihimili miwili iliyobakia yaani Bunge na Mahakama. Hivyo cheo cha Rais nchini Iran ni muhimu sana na bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza tena jana kwamba, kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi huo ni jambo la wajibu.

342/