Kulingana na ripoti ya Shirika la Habari la Iran (IRNA), Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Ali Bagheri Kani, katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov, ameashiria mafanikio ya hivi karibuni katika ushirikiano wa pande mbili za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia hususan kutiwa saini hati ya maelewano ya kusafirisha gesi ya Russia hadi Iran.
Amesema mwenendo wa uhusiano wa nchi mbili uko katika mwelekeo sahihi na unakwenda kwa kasi inayofaa. Kuhusu mpango wa Moscow wa kujadili kadhia ya Palestina na jinai zilizofanywa na Wazayuni huko Gaza katika kipindi cha urais wa zamu wa Russia katika Baraza la Usalama mwezi Julai mwaka huu, Ali Bagheri Kani ametangaza utayarifu wa Iran kushiriki katika vikao husika katika ngazi ya juu kabisa. Kwa upande wake, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia ameeleza kuridhishwa kwake na mchakato wa ushirikiano wa pande mbili, na kusema Moscow inazingatia suala la kupeleka mbele ajenda hiyo kwa kushirikiana na Iran. Sergei Lavrov ameashiria wasiwasi wa Russia kuhusu uwezekano wa kupanuka wigo wa vita na uchokozi wa Wazayuni hadi Lebanon na kusema, Moscow inataka kuzuia jambo hilo na inasisitiza wajibu wa pande zote katika suala hilo.
342/