Ali Bagheri Kani amesema hayo pambizoni mwa kikao cha leo cha serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, kutokana na nguvu za kambi ya muqawama, Lebanon ina ushawishi na nafasi muhimu hata ya kisiasa na kidiplomasia kama ambavyo pia, muqawama umeiletea kinga ya kutoshambuliwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Amma kuhusu safari ya Mrithi wa Kiti ya Ufalme wa Saudia hapa nchini Iran, Bagheri amesema kuwa, safari yake hiyo imo katika ajenda ya serikali mbili za Iran na Saudia, kinachosubiriwa ni kuona ni serikali gani taingia madarakani nchini Iran baada ya uchaguzi wa duru ya pili ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu wa keshokutwa Ijumaa.
Kaimu huyo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vile vile amesema kuhusu uwezekano wa kurejea madarakani Donald Trump nchini Marekani kwamba, muundo wa nguvu na uwezo wa Jamhuri ya Kisilamu ni mkubwa kiasi kwamba, kuingia na kutoka viongozi mbalimbali iwe ni Rais au kiongozi mwingine yeyote hakubadilishi siasa za kiistratijia za Iran. Aidha amesema, tab'an Iran imejiwekea mikakati madhubuti ya kuifuata kimataifa kulingana na mazingira yanayojitokeza ulimwenguni.
342/