Main Title

source : Parstoday
Jumatano

3 Julai 2024

17:20:37
1469400

Mkutano wa "AALCO" mjini Tehran: Ugaidi ndio mada kuu ya mijadala

Mkutano wa kikanda wa Jumuiya ya Ushauri wa Kisheria ya Asia na Afrika (AALCO) unafanyika mjini Tehran kwa lengo la kuchunguza njia za kupambana na ugaidi.

Mkutano huo ulioanza leo mjini Tehran utaendelea hadi kesho Alkhamisi. Mkutano huo unahudhuriwa na wawakilishi wa AALCO, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na wataalamu kutoka nchi mbalimbali duniani.

Mambo yanayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na "kuzuia na kukabiliana na ugaidi kuanzia nadharia hadi vitendo", "jukumu la mashirika ya kimataifa na ya kikanda katika kuzuia na kupambana na ugaidi", "wajibu wa serikali na watu binafsi kuhusiana na ugaidi", "ushirikiano wa kikanda katika kuzuia na kupambana na ugaidi", maoni na mitazamo ya kisheria ya kimataifa ya nchi wanachama wa AALCO, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuhusu kuzuia na kukabiliana na ugaidi, na vilevile suala la kukabiliana na kuzuia ugaidi kwa mtazamo ya nchi za Asia na Afrika.

Asian-African Legal Consultative Organization (AALCO) ni taasisi ya kisheria inayotokana Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), ambayo lengo lake muhimu zaidi ni ushirikiano wa nchi za Asia na Afrika kwa ajili ya kutatua matatizo yanayohusu masuala ya kisheria ya kimataifa, na uratibu na makubaliano ya nchi wanachama kuhusu baadhi ya masuala ya kisheria ya kimataifa. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Pakistan, Libya, Oman, Korea Kusini, Nigeria, Tanzania, pamoja na Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi wanachama wa "AALCO.

Mkutano wa sasa wa AALCO mjini Tehran umejikita zaidi kwenye suala la ugaidi na njia ya kukabiliana nao. Kufanyika mkutano huu mjini Tehran kunaonyesha umuhimu na nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kupambana na makundi ya kigaidi ya kitakfiri katika eneo la Magharibi mwa Asia, katika miaka ya hivi karibuni. 

Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani na nchi nyingine za Magharibi, zimetumia vibaya hali ya eneo la Magharibi mwa Asia na kuingilia masuala ya ndani ya nchi za eneo hilo, na zimetuma vikosi vyao vya kijeshi huko Syria na Iraq kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Sambamba na hayo, makundi ya kigaidi nayo yametumia fursa hiyo kuzidisha hali ya ukosefu wa amani Magharibi mwa Asia kwa kutumia mazingira yaliyojitokeza. 

Katika kutekeleza siasa zake za kuimarisha amani na usalama, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepanua ushirikiano wake na nchi za eneo hili ili kukabiliana na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS). Sera hizo za kikanda za Iran zimeimarisha usalama na amani na kupongezwa na nchi mbalimbali. Sera hizo za Iran zimeyalazimisha makundi ya kigaidi kukimbia na mengine kusambaratika.
Uzoefu wa matukio ya karibuni katika kanda ya Asia Magharibi umeonyesha haja ya nchi mbalimbali kushirikiana kadiri inavyowezekana, na kuepuka kuingiliwa na mataifa ya kigeni. Mkutano wa kilele wa AALCO ni nembo ya ushirikiano wa nchi huru na zinazojitawala kwa ajili ya kukabiliana na makundi ya kigaidi. Kufanya mikutano ya kilele kama huu wa AALCO kunaweza kuharakisha mchakato wa ushirikiano wa kikanda katika fremu ya kupambana na ugaidi na kukata mikono ya madola ya ajinabi na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na madola hayo. Ushirikiano huu pia unaweza kuwa mwanzo wa kuzuia uingiliaji kati wa nchi za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi huru na kupanua wigo wa ushirikiano wa nchi jirani na zinazojitawala.


342/