Takwimu zilizochapishwa na Ofisi ya Takwimu ya Uturuki zinaonyesha kuwa, mabadilishano ya kibiashara ya Iran na nchi hiyo yamefikia dola bilioni mbili na milioni 300 na ukuaji wa 5% katika miezi mitano ya mwanzo ya mwaka huu.
Pia, kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na Kituo cha Takwimu cha Ulaya (Eurostat), kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minne iliyopita Uturuki imeagiza bidhaa za mafuta au mafuta kutoka Iran.
Nchi hiyo imeagiza tani 576 za mafuta au bidhaa za mafuta kutoka Iran mwezi Machi mwaka huu na tani 485 mwezi Aprili ikiwa ni jumla ya tani 1060. Kwa mara ya mwisho Uturuki iliingiza kutoka Iran shehena ya mafuta mnamo Agosti 2020.
Katika safari ya shahidi Ebrahim Raisi nchini Uturuki yapata miezi 5 iliyopita, hati 10 za ushirikiano zilitiwa saini baina ya pande mbili katika nyanja mbalimbali zikiwemo sayansi na teknolojia, usafirishaji na uchukuzi, nishati, mafuta na gesi, petrokemikali, umeme, maeneo huria ya biashara, utamaduni, vyombo vya habari na mawasiliano na baadhi ya maeneo mengine, na hivi sasa inaonekana kwamba, hati hizi ziko katika hatua za utekelezaji.Mwezi wa tano mwaka huu, Uturuki ilisafirisha bidhaa za dola milioni 285 kuja Iran na kuagiza bidhaa za dola milioni 262 kutoka Iran. Mauzo ya Uturuki kwa Iran mwezi Mei mwaka huu yaliongezeka kwa 14% ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, na uagizaji wa nchi hiyo kutoka Iran pia uliongezeka kwa 20%. Mnamo Mei 2023, Uturuki ilisafirisha bidhaa za dola milioni 249 kuja Iran na kuagiza bidhaa za dola milioni 217 kutoka Iran.
Mabadilishano ya kibiashara ya Iran na Uturuki yalifikia dola bilioni 5 na milioni 490 mwaka 2023. Mwaka huu, Uturuki ilisafirisha nje bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 3 na milioni 310 kuja Iran na kuagiza bidhaa za thamani ya bilioni 2 na milioni 180 kutoka Iran.
Baada ya biashara kati ya Iran na Uturuki kufikia dola bilioni 22 mwaka 2012, nchi hizo mbili ziliamua kuongeza kiwango cha biashara baina yao hadi kufikia dola bilioni 30. Pamoja na hayo, uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili ulifikia dola bilioni 6.4 mnamo 2022.
Miongoni mwa vizingiti vinavyokwamisha uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili ni pamoja na udhaifu wa miundo mbinu ya barabara na reli, ukaguzi wa mpakani wa bidhaa na kuharibika mizigo, hatua kali zinazochukuliwa dhidi ya vyombo vya usafiri na kulazimika kubadili njia, foleni ndefu kwenye vituo vya ukaguzi na kadhalika masuala ambayo yamekuwa yakiongeza gharama.
Katika miaka ya hivi karibuni, Uturuki imekuwa ikizingatiwa kuwa mshirika muhimu wa kibiashara wa Iran, na katika kipindi cha miaka 10 iliyopita daima imekuwa miongoni mwa nchi 5 za juu katika vyanzo vikuu vya usafirishaji na uingizaji wa bidhaa za Iran, na tangu 2016 imeweza kujiimarisha kama mojawapo ya maeneo 5 muhimu zaidi ya bidhaa za Iran.Uchunguzi kuhusiana na hali ya uhusiano kati ya Iran na Uturuki unaonyesha kuwa, ijapokuwa historia ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili inafikia zaidi ya miaka 400 na zina mafungamano katika nyanja za kisiasa, kiutamaduni, kihistoria na kidini, na kuna zaidi ya kilomita 500 za pamoja mpaka kati ya Iran na Uturuki, lakini katika nyanja ya kiuchumi na kibiashara, bado kuna uwezo mwingi ambao haujatumika. Hii ni pamoja na kwamba, kwa mujibu wa msisitizo wa wataalamu, Uturuki inaweza kuwa daraja la kuunganisha kati ya Iran na Ulaya, na kwa upande mwingine, Iran inaweza kuwa moja ya barabara zinazounganisha Uturuki na njia nyingine kama na India na kadhalika. Kwa kweli, kwa kutumia uwezo huu, nchi hizo mbili zinaweza kuandaa msingi wa ustawi na maendeleo yao ya kiuchumi kupitia uwekezaji wa pamoja na mauzo ya nje ya bidhaa zinazozalishwa kwa pamoja kwa nchi za tatu. Mabunge ya nchi hizo mbili, ambayo yana jukumu la kuanzisha ushuru wa upendeleo, yanaweza kuidhinisha ushuru huu ili wafanyabiashara wa Iran na Uturuki waweze kufanya kazi kwa urahisi. Katika miongo kadhaa iliyopita, Uturuki na Iran zimejaribu kuepusha mivutano mikubwa ya kijeshi na kisiasa kati yao na kuweka kipaumbele katika maendeleo ya uhusiano wa kiuchumi, kibiashara, kiutamaduni, kisayansi na kiutalii. Mataifa ya Iran na Uturuki pia yamefikia maelewano ya pamoja ya kunufaishana kupitia biashara na hata kuunda mtaji, jambo ambalo linatoa uungaji mkono mkubwa kwa mchakato unaokua wa mahusiano ya kibiashara na kiuchumi kati ya Iran na Uturuki.
342/